Biden akutana na viongozi wa Ufilipino na Japan
12 Aprili 2024Rais wa Marekani Joe Biden ameapa kuilinda Ufilipino dhidi ya shambulio lolote katika Bahari ya Kusini mwa China, wakati alipokuwa mwenyeji wa mkutano wa kwanza wa pamoja wa viongozi wa Japan na Ufilipino katikati mwa mvutano na China.
Mkutano huo wa pande tatu wa Biden na Rais wa Ufilipino Ferdinand Marcos na Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida unafuatia makabiliano ya mara kwa mara kati ya meli za China na Ufilipinokatika njia hiyo ya maji inayozozaniwa.
Biden ameongeza kuwa shambulio lolote dhidi ya meli za Ufilipino au vikosi vya kijeshi katika Bahari ya Kusini mwa China, kutachochea matumizi ya mkataba wa pamoja wa ulinzi wa pande zote.
China inadai kuwa eneo zima la Bahari ya China Kusini ni himaya yake, ikipuuza madai kutoka kwa mataifa kadhaa ya Kusini Mashariki mwa Asia ikiwa ni pamoja na Ufilipino.
Mkutano huo wa pamoja umefanyika siku moja baada yaBiden kufanya mazungumzo na waziri mkuu wa Japan Fumio Kishida na kubainisha mipango ya ushirikiano wa kiusalama katika kukabiliana na China inayozidi kujiimarisha.
Kishida alitoa hotuba ya pamoja kwa bunge la Marekani siku ya Alhamisi ambapo aliwataka Wamarekani kuondokana na "mashaka" kuhusu jukumu lao kama taifa lenye ngumu kimataifa.
Katika mkutano wa kilele wa pande tatu, Marekani, Japan na Ufilipino zinatarajiwa kutangaza luteka mpya za pamoja za jeshi la wanamaji pamoja na Australia, sawa na mazoezi waliyofanya katika eneo hilo mwishoni mwa juma.
Japan na Ufilipino ni washirika wa hivi karibuni zaidi wa kanda ya Asia-Pasifiki kualikwa na Biden, ambaye alikutana na Kishida na Rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol mnamo Agosti.Japan na Marekani zakubaliana kuimarisha ushirikiano wa kiusalama
Rais Biden pia alitafuta kupunguza mvutano na China, baada ya kufanya mazungumzo ya simu na Rais Xi Jinping wiki iliyopita kufuatia mkutano wa ana kwa ana huko San Francisco mnamo mwezi Novemba.