1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Benki ya dunia yafungua ofisi mpya mjini Berlin

Josephat Charo6 Novemba 2007

Benki ya dunia, taasisi muhimu katika maswala ya misaada ya maendeleo, jana ilifungua ofisi yake ya kwanza mjini Berlin hapa Ujerumani. Rais wa benki ya dunia, Robert Zoellick, na waziri wa misaada ya maendeleo wa Ujerumani, Heidermarie Wieczoreck-Zeul, walihudhuria sherehe ya ufunguzi wa ofisi hiyo.

https://p.dw.com/p/C7f7
Heidermarie Wieczoreck-Zeul (kushoto) na Robert Zoellick
Heidermarie Wieczoreck-Zeul (kushoto) na Robert ZoellickPicha: AP

Rais wa benki ya dunia, Robert Zoellick, alisema Ujerumani iko msitari wa mbele katika misaada ya maendeleo. Bwana Zoelllick ana matumaini kwamba ofisi ya mjini Berlin itasaidia kuwapata washirika wa kuzungumza nao katika maswala ya kisiasa, kiuchumi na vyombo vya habari.

Waziri wa misaada ya maendeleo wa Ujerumani, Heidermarie Wieczoreck-Zeul, na rais mpya wa benki ya dunia, Robert Zoellick, wanaziona juhudi za kupambana na umaskini duniani zikiwa katika kasi nzuri. Waziri Wieczoreck-Zeul alisema wakati wa sherehe ya ufunguzi ya ofisi ya benki ya dunia mjini Berlin hapo jana kwamba kuna maswala makubwa ya kisiasa ambayo yanatakiwa kusawazishwa katika shirika la ushirikiano wa kiufundi la Ujerumani, GTZ la mjini Berlin.

Heidermarie Wieczoreck-Zeul alisema ipo haja ya kuungana pamoja katika vita dhidi ya umasikini barani Afrika. Aidha kiongozi huyo alisema ipo haja ya kuboresha mazingira na kuziongezea nguvu juhudi za utoaji wa huduma za afya, kuwepo na mifumo ya kibiashara itakayofanya kazi vizuri, na juu ya yote kuyalinda mazingira.

´Tumekubaliana juu ya udhamini wa juhudi hizi wakati huo huo kuupa kipaumbele udhamini wa upatikanaji wa nishati endelevu katika nchi zinazoendelea. Na pia kuchangia kuona kwamba kuna msaada kwa nchi ambazo zina misitu inayokua katika maeneo ya joto.´

Rais wa benki ya dunia, Robert Zoellick alikumbuka ziara yake ya kwanza mjini Berlin baada ya kuchukua hatamu za uongozi katika benki hiyo mnamo mwezi Julai mwaka huu, na kuzungumzia ahadi zilizotolewa na nchi zilizoendela zaidi kiviwanda duniani za G8 wakati wa mkutano wao katika mji wa Heiligendamm mwanzoni mwa msimu uliopita wa kiangazi mwaka huu. Wakati huo kulikuwa na matumiani makubwa miongoni mwa nchi zinazoendelea.

´Na kuna hofu miongoni mwa nchi za Afrika kwamba raslimali za maendeleo zitaelekezwa katika juhudi za kupambana mabadiliko ya hali ya hewa badala ya kuendeleza maendeleo. Na hiyo ndiyo sababu kwa nini muhimu kuyasaidia mashirika ya misaada.´

Aidha bwana Zoellick amesema, ´Pili kuna hofu kwamba itabana maendeleo. Sidhani kuwa hii ndiyo hali inayotakiwa kuwepo. Nimekuwa nikifanya kazi pamoja na mwenyeji wa mkutano Indonesia na sababu moja kwa nini mimi na waziri Zeul tumekubali kwenda Bali, ni kuonyesha ishara za juhudi za kujumulisha pamoja maendeleo na mabadiliko ya hali ya hewa kama swala muhimu.´

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa umepangwa kufanyika katika kisiwa cha Bali nchini Indonesia mwezi ujao wa Disemba. Rais wa benki ya dunia, Robert Zoellick, na waziri wa misaada ya maendeleo wa Ujerumani, Heidermarie Wieczoreck- Zeul, wameonya kabla mkutano juu ya nchi zinazochipuka kiuchumi kama vile China na India, zisipuuzie juhudi za kuyalinda mazingira.

Ukizingatiwa ukuaji wa kasi wa kiuchumi katika nchi hizo na ongezeko kubwa la mahitaji ya nishati ipo haja ya kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi hayasababishi athari za kijamii na kimazingira.