1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Benki ya Dunia: Umaskini uliokithiri utaendelea kuwepo

6 Oktoba 2022

Benki ya Dunia imesema sio rahisi ulimwengu kulifikia lengo lake la kuondoa umaskini uliokithiri ifikapo mwaka 2030, huku wataalamu wakisema janga la COVID-19 limekwamisha juhudi za kupunguza umaskini kwa miongo kadhaa.

https://p.dw.com/p/4HoSu
Symbolbild I Armut
Picha: Eranga Jayawardena/AP/picture alliance

Hayo yameelezwa katika ripoti mpya ya Benki ya Dunia iliyopewa jina ''Umaskini na Ustawi wa Pamoja'' ambayo inaelezea maendeleo katika juhudi za kimataifa za kumaliza umaskini uliokithiri. Ripoti hiyo iliyotolewa Jumatano imelitaja janga la virusi vya corona kama kizuizi kikubwa katika juhudi za kupunguza umaskini duniani kwa miongo kadhaa.

2020 watu waliishi kwa dola 2.15 kwa siku

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, mwaka 2020 ulishuhudia zaidi ya watu milioni 71 wakiishi kwa dola 2.15 kwa siku au chini ya hapo, na kufikisha idadi jumla ya watu milioni 719 ambayo ni sawa na takribani asilimia 9.3 ya idadi ya watu ulimwenguni.

Wachumi wa benki hiyo wamesema hali imekuwa mbaya zaidi baada ya Urusi kuivamia Ukraine, pamoja na kusuasua kwa uchumi wa China, mfumuko wa bei na kuongezeka kwa bei ya chakula na nishati, hatua ambazo zinaendelea kukwamisha maendeleo katika siku zijazo.

David Malpass
Rais wa Benki ya Dunia, David MalpassPicha: Indraneel Chowdhury/NurPhoto/picture alliance

Ripoti hiyo imesema bila ya kuwepo ukuaji wa kasi wa uchumi, watu wapatao milioni 574 ambao ni sawa na asilimia 7 ya idadi ya watu ulimwenguni bado wataendelea kuishi katika umaskini uliokithiri mwaka 2030.

Rais wa Benki ya Dunia, David Malpass amesema ripoti hiyo inaonesha hali mbaya inayowakabili mamilioni ya watu na ametoa wito wa kufanyika mabadiliko makubwa ya sera ili kuongeza ukuaji na kusaidia juhudi za haraka za kutokomeza umaskini.

Nchi zilizoendelea zipunguze matumizi

''Pamoja na mfumuko wa bei kuwa juu, nchi zilizoendelea kiuchumi zipunguze ukubwa wa matumizi ya sasa ya serikali na kuimarisha ufanisi kwa kuwalenga zaidi maskini na walio katika hatari. Hii itapunguza mahitaji yasiyo na tija na kuacha nafasi zaidi kwa masoko ya mitaji ya kimataifa kufadhili uwekezaji na kuondoa shinikizo la mfumuko wa bei,'' alisisitiza Malpass.

Kwa mujibu wa Malpass mafanikio katika kupunguza umaskini uliokithiri kimsingi yamesimama sanjari na ukuaji duni wa uchumi duniani. Amesema mfumuko wa bei, kushuka kwa thamani ya sarafu na migogoro mikubwa inayoingiliana, inachochea umaskini zaidi.

Welternährungsprogramm der Vereinten Nationen
Watu wa Sudan Kusini wakisubiri chakula kutoka katika Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFPPicha: Maciej Moskwa/NurPhoto/picture-alliance

Wachumi wamebainisha kuwa asilimia 60 ya umaskini uliokithiri unapatikana Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambako kuna kiwango cha umaskini cha asilimia 35.

Kwa ujumla umaskini duniani ulishuka kutoka asilimia 38 mwaka 1990, wakati Benki ya Dunia ilipoanza kuufuatilia, hadi asilimia 8.4 mwaka 2019. Hata hivyo, janga la COVID-19 limechochea kuongezeka kwa umaskini uliokithiri kwa mara ya kwanza kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita.

Mchumi Mkuu katika Benki ya Dunia, Indermit Gill amesema katika muongo ujao, kuwekeza katika huduma bora ya afya na elimu, itakuwa muhimu kwenye nchi zinazoendelea kiuchumi. Ripoti hiyo imehitimisha kuwa lengo la kuutukomeza umaskini ifikapo mwaka 2030, bado haliwezi kufikiwa.

(AFP, Reuters, DW)