Beijing yatoa masharti kabla ya mkutano wa Xi na Biden
13 Novemba 2023Msemaji wa Wizara ya Mambo ya nje ya China Mao Ning amesema mjini Beijing kwamba Marekani inapaswa kuheshimu wasiwasi halali unaoonyeshwa na China na haki ya watu wake kujiendeleza badala ya kuzingatia namna ya kuvuruga maslahi ya China.
"Ushindani wa mataifa makubwa hauendani na mwelekeo wa nyakati hizi na hauwezi kutatua matatizo ya Marekani au changamoto zinazoukabili ulimwengu. China haiogopi ushindani, ila tunachopinga ni kuuelezea uhusiano kati ya China na Marekani kwa maneno ya ushindani. Linapokuja suala la wasiwasi, Marekani inapaswa kuheshimu kwa dhati wasiwasi wa China na haki halali za maendeleo, badala ya kusisitiza tu masuala yake huku ikiathiri maslahi ya China," alisema Mao Ning, msemaji wa Wizara ya Mambo ya nje ya China.
Mkutano wa kilele wa APEC wafanyika tena Marekani baada ya zaidi ya miaka 10
China imesema inatumaini kwamba Marekani haitaki Vita Baridi ama mzozo na watu wa China na badala yake itarejesha uhusiano mzuri baina yao, wakati rais Xi Jinping na Joe Biden wakitarajiwa kukutana ana kwa ana pembezoni mwa mkutano wa kilele wa Ushirikiano wa Mataifa ya Asia na Pasifiki, APEC, siku ya Jumatano.