1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern yafungwa na Manchester City katika mechi ya kirafiki

26 Julai 2023

Beki wa Manchester City Aymeric Laporte aliifungia klabu hiyo bao la ushindi kunako dakika za lala salama walipoibwaga Bayern Munich mabao 2-1 katika mechi ya kujipima nguvu kuelekea msimu mpya iliyochezwa mjini Tokyo.

https://p.dw.com/p/4UQWZ
Fußball Bayern München v Manchester City | Erling Haaland
Mshambuliaji wa Manchester City Erling Haaland.Picha: Joe Robbins/Icon Sportswire/IMAGO

Ushindi huo wa Manchester City ni wa pili mfululizo katika mechi zao za kirafiki baada ya wiki iliyopita kuipa kichapo Yokohama F. Marinos cha magoli 5-3.

Pep Guardiola aliweka kikosi imara cha kwanza akiwemo Kyle Walker anayemezewa mate na Bayern Munich.

Kinda James McAtee, ambaye msimu uliopita aliichezea Sheffield United kwa mkopo ndio aliyefungua ukurasa wa mabao kwa kupachika goli kunako dakika ya 21 ya mchezo.

Champions League | Viertelfinale | Manchester City vs Bayern München
Kiungo wa Manchester City Rodrigo akifunga bao katika pambano la robo fainali ya Ligi Mabingwa dhidi ya Bayern Munich msimu uliopita ugani Ettihad.Picha: Jon Super/AP Photo/picture alliance

Pep Guardiola na Thomas Tuchel walifanya mabadiliko mengi baada ya kipindi cha kwanza huku Bayern Munich ikisawazisha kupitia Mathy Tel kabla ya hatimaye Laporte kufunga bao la pili na la ushindi.

Mabingwa hao wa Ulaya na Ligi Kuu ya Premia sasa wanaelekea mjini Seoul, Korea Kusini kuzipiga na Atletico Madrid katika mechi yao ya mwisho ya kirafiki mnamo siku ya Jumapili.

Vijana wa Pep Guardiola watateremka tena uwanjani Wembley kumenyana na washika bunduki Arsenal katika mchezo wa ngao ya jamii Agosti 6.

Bayern kwa upande bado watasalia Tokyo, ambapo wameratibiwa kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya klabu ya Ligi Kuu ya Japan Kawasaki Frontale siku ya Jumamosi katika maandalizi kuelekea msimu mpya wa Bundesliga.