1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makocha wa Premier League waimarisha kikosi cha England

Sekione Kitojo
11 Juni 2018

Utandawazi katika ligi ya England mara nyingi umelalamikiwa kuzuwia mafanikio ya wachezaji wa ndani lakini uwepo wa makocha kama  Pep Guardiola na Juergen Klopp umesababisha kuimarisha nafasi ya Uingereza kombe la dunia.

https://p.dw.com/p/2zJ01
Fußball Premier League Jürgen Klopp und Pep Guardiola
Picha: picture-alliance/dpa/AP Photo/R. Vieira

Katika kikosi  cha  kocha  Gareth Southgate cha  wachezaji  23 nchini  Urusi,  15 walimaliza  katika  timu  zilizoko  katika  nafasi  nne za  juu  chini  ya  makocha  nyota Guardiola, Klopp, Jose Mourinho na  Mauricio Pochettino.

Pep Guardiola
Picha: picture-alliance/empics/N. Potts

Manchester  City imevunja  rekodi  kadhaa  za   Premier League wakati  wakielekea  katika  ubingwa  wao  msimu  huu, ambapo Raheem Sterling , Kyle Walker, John Stones  na  Fabian Delph wakionekana   bila  shaka  yoyote  wakiongeza  viwango  vyao  chini ya  kocha  Pep Guardiola.

"Bila  shaka,"  Delph  aliliambia  shirika  la  habari  la  AFP wakati alipoulizwa  iwapo  kocha  wake  kutoka  jimbo  la  Catalonia  alikuwa ufunguo  wa  kuchaguliwa  kwake  katika  kikosi  cha  England. "Kwangu  mimi  ni  mtu  mwenye  kipaji  cha  hali  ya  juu  kabisa."

Mchezaji  ambaye  kawaida  hucheza  kama  kiungo  wa  kati, Delph kwa  muda  mrefu  wa  msimu  alichezea   beki  wa  kushoto  wakati Guardiola  alitumia  uwezo  wake  na  kumpa  majukumu  mapya.

"Amefungua  macho  yangu  kuona  mambo  mengi. Kuwahi  kufikiria kuhusu  kandanda  kama  Pep  anavyofikiria," alisema  Delph . "Kimsingi  mimi  ni  Muingereza  halisi. Naamini  katika  kufanya  kazi ngumu  na  dhamira  thabiti na  kujitolea  kwa  kila  kitu. Unafahamu kwamba  niko  hapa  kupambana, kutafuta  mipira  inayorudi  ya  pili na  kuwa  mfano  wa  kizamani  wa  Mwingereza.

"Sasa  inahusiana  zaidi  na  kuwa  mtulivu na  kuwa  makini unapokuwa  na  mpira."

Fußball Premier League Jürgen Klopp und Pep Guardiola
Kocha Pep Guardiola (kulia) na Jurgen Klopp (kushoto)Picha: picture-alliance/dpa/AP Photo/D. Zhompson

Southgate  anaamini  Guardiola alikuwa   anashawishi  utaratibu wake  wa  kucheza  kandanda  kabla  ya  kuwasili  nchini  Uingereza, kutokana  na  kikosi  chake  cha  ajabu  cha  Barcelona ambacho kilishinda  mataji  mawili  ya  Champions League  katika  muda  wa miaka minne ya  fahari  kati  ya  mwaka  2008  na  2012.

Athari za Barcelona

"Athari  zilizotokana na  kuiona  timu  ya  Barcelona  miaka mitano  hadi  saba iliyopita ilikuwa  kubwa,"  amesema  Southgate. "Amekuwa mgunduzi. Wakati  nikiangalia  mpira  wa  watoto  hii  leo, wakati wakiingia  katika  viwnja  ambavyo  havikujaa  maji  ama  kuganda barafu, nawaona  wakicheza  wakianzia  nyuma.

 

"Siwaoni makocha   vichwa  vyao  vikiwa  katika  mikono  yao wakisema , "peleka  mbele". Nafikiri  hii  ni  athari  ya  timu  yake, ikiwa  na  wachezaji  kama  Andres Iniesta  na  Xavi."

Hata  hivyo , Guardiola  sio  kocha  pekee ambaye  ameisaidia England  kufanya  vizuri. Stones , Walker  na  Sterling  walikuwa tayari  wachezaji  wa  timu  ya  taifa  kabla  ya  kupelekwa  katika kiwango  kingine  na  kocha  huyo  wa  zamani  wa  Barca  na Bayern Munich.

Großbritannien Mauricio Pochettino, Manager Tottenham Hotspur
kocha wa Tottehmam PochettinoPicha: Getty Images/M. Regan

Kwa  ulinganisho, Pochettino  wa  Tottenham  amewaendelea  wengi wa  wachezaji   nyota wa  Southgate  kama  harry Kane  na  Dele Alli  kutoka  katika  kiwango  chao  cha  awali, na  kuwabadilisha kutoka  wachezaji  ambao  hawana  majina  kuwa  wachezaji  wenye majina  makubwa. Danny Rose , Eric Dier  na  Kieran Trippier wanakamilisha  kundi  la  wachezaji  watano  wa  Spurs  katika kikosi  kilichoko  nchini  Urusi na  wamekuwa wakisisitiziwa  kucheza katika  misingi  ya  udhibiti wa  kandanda  na  kuweka  mbinyo ambako  Guardiola  anahubiri  kila  mara.

Athari  za  Klopp

Trent Alexander-Arnold  ameanza  kuichezea kwa  mara  ya  kwanza England  katika  ushindi  wa  mabao 2-0  katika  mchezo wa  kirafiki dhidi  ya  Costa  Rica baada  ya  kucheza  vizuri  katika  msimu  huu chini  ya  Klopp  na  kumalzikia  katika  fainali  ya  Champions League  dhidi  ya  Real  Madrid  pamoja  na  nahodha  wa  Liverpool na  mchezaji  mwenzake  katika  kikosi  cha  England Jordan Henderson.

"Kama wachezaji wamepata fursa kubwa  ya  kucheza  chini  ya kocha  kama  huyo, kwasababu  unajifunza  mengi  kutoka  kwake," amesema  Henderson, akimaanisha  athari  za  Klopp.

England Training und Pressekonferenz - Tottenham Hotspur Football Club Trainingsgelände
Kocha wa Uingereza Gareth SouthgatePicha: picture-alliance/D.Klein

Mourinho  amewapa  nidhamu  ya  ulinzi Ashley Young  na kumbadilisha  kijana  huyo  mwenye  umri  wa  miaka 32  ambaye hapo  kabla  alikuwa  mshambuliaji  wa  pembeni  na  kuwa  mlinzi wa  kushoto ambaye  kocha  Southgate  anamuona  ni  muhimu sana  kwa  kikosi  chake  kuliko Ryan Bertrand, ambaye  amecheza mara  tano  katika  duru za  mchujo.

Na Jesse Lingard  anatoa  changamoto  kwa  dhana  kwamba Mourinho  hatoi  nafasi kwa  vijana  na  alifunga  mabao 13  katika msimu  wake  mzuri  kabisa  akiwa  na  Manchester  United na  kutoa changamoto  kwa  kocha  kumpanga  katika  kikosi  cha  kwanza katika  mchezo  wake  wa  ufunguzi  dhidi  ya  Tunisia  katika  kundi G.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Mohammed  Abdul Rahman