1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUfaransa

Barnier aanza kukabiliana na vizingiti vya kuunda serikali

6 Septemba 2024

Waziri Mkuu mpya wa Ufaransa Michel Barnier ameanza kushauriana na pande za kisiasa nchini humo ili kuunda serikali itakayokuwa na wingi bungeni, baada ya miezi miwili ya mkwamo wa kisiasa.

https://p.dw.com/p/4kM2o
Ubelgiji Brüssel 2017 | Michel Barnien, Brexit
Waziri Mkuu mpya wa Ufaransa Michel BarnierPicha: Emmanuel Dunand/AFP/Getty Images

Barnier aliyeteuliwa jana na Rais Emmanuel Macron, tayari amesema atatekeleza wajibu wake mpya kwa kuzingatia "utu".

Amevitaja vipaumbele vyake kuwa ni elimu, usalama na udhibiti wa uhamiaji na kuongeza kuwa hataogopa kuzungumza ukweli kuhusiana na deni la taifa, huku akiahidi mageuzi.

"Ninawaza mabibi na mabwana kila mmoja kupata huduma za umma, shule zitaendelea kuwa kipaumbele cha Serikali, shule za umma. Nafikiria usalama wa kila siku, nafikiria pia kudhibiti uhamiaji. Ninafikiria, bila shaka, juu ya ajira na hali ya maisha ya Wafaransa."

Barnier, aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na mpatanishi wa Umoja wa Ulaya kwenye mchakato wa Brexit, ameteuliwa baada ya wiki kadhaa za mkwamo kufuatia uchaguzi wa mapema ambao haukutoa mshindi wa moja kwa moja.