1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barcelona yaachwa hoi Champions League, kocha ajitetea

16 Septemba 2021

Kocha wa Barcelona Ronald Koeman amesikitishwa na matokeo mabaya ya timu yake baada ya kupokea kichapo cha mabao 3-0 na Bayern Munich katika michuano ya ligi ya mabingwa barani ulaya Champions League.

https://p.dw.com/p/40OBx
Champions League | FC Barcelona vs. FC Bayern München | Trainer
Picha: Albert Gea/REUTERS

Koeman amewataka mashabiki kuelewa kuwa timu hiyo inapitia kipindi cha mpito.

Kocha huyo raia wa Uholanzi ameelezea hali ya majeruhi katika kikosi chake ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa washambuliaji Ousmane Dembele, Ansu Fati, Martin Braithwaite na Sergio Aguero na kusisitiza kuwa, hata beki Jordi Alba aliingia uwanjani licha ya kuwa mgonjwa siku moja kabla ya mechi hiyo.

Soma zaidi: Messi ni mchezaji rasmi wa PSG sasa

Katika mkutano na waandishi habari Koeman alisema "Mnatakiwa kukubaliana na hali halisi maishani. Wachezaji wetu vijana wameonyesha kuwa tuna mustakabali mzuri na pia tuna wachezaji wengi waliorejea mazoezini baada ya majeraha. Ndivyo ilivyo."

" Hakika ni vigumu sana kucheza na timu kama Bayern Munich wakati hamna kasi ya kutosha ya kushambulia. Lazima tukubaliane na matokeo na tuendelee kuchapa kazi lakini pia kuna umuhimu wa kuitambua timu pinzani. Ili kuishinda timu kama Bayern, lazima uwe katika ubora na tunatakiwa kukubali wakati washindani wetu wako vizuri."

Timu ya Barcelona haikufanikiwa kulishambulia hata mara moja lango la Bayern katika mchezo huo uliochezwa mnamo siku ya Jumanne.

Bayern ilijipatia mabao yao kupitia Thomas Muller na Robert Lewandowski aliyefunga mabao mawili.

Hii si mara ya kwanza kwa Bayern kuifunga Barcelona, kwani misimu miwili iliopita iliifunga Barcelona mabao 8-2 katika hatua ya robo fainali ya Champions League.

Barcelona itaingia tena uwanjani Jumatatu ijayo Septemba 20 katika ligi kuu ya Uhispania La Liga, itakapochuana na Granada. Timu hiyo inashikilia nafasi ya saba kwenye jedwali la Liga linaloongozwa na Real Madrid.