1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroKimataifa

Baraza kuu la UN laitaka Urusi kuondoa majeshi yake Ukraine

Sylvia Mwehozi
24 Februari 2023

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio lisilofungamana linaloitaka Urusi kukomesha mapigano nchini Ukraine na kuondoa mara moja vikosi vyake, huku nchi saba zikipinga azimio hilo.

https://p.dw.com/p/4NvZB
UN-Generalversammlung stimmt über Reparationsantrag für die Ukraine ab
Picha: Michael M. Santiago/Getty Images

Azimio hilo lililoandaliwa na Ukraine pamoja na washirika wake, limepitishwa kwa kura 141 za ndiyo, 7 za hapana na nchi 32 zikijuzuia. Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba amesema kuwa kura hiyo ilikuwa ni ushahidi wa kutosha kwamba si mataifa ya Magharibi pekee ambayo yanaiunga mkono nchi yake.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield alisema kuwa; "na kama ilivyoelezwa katika azimio la Ukraine, nchi hizi 141 zilisisitiza matakwa ya wazi kwa Urusi kujiondoa. Ondoka mara moja na bila masharti kutoka katika eneo linalotambulika kimataifa la Ukraine. Rudisha askari wako nyumbani na ukomeshe vita hivi."

Mawaziri wa mambo ya kigeni na wanadiplomasia kutoka nchi zaidi ya 75 walihutubia hadhara ya baraza hilo wakati wa kikao cha siku mbili huku wengi wakielezea uungwaji mkono wa azimio linalotetea ulinzi wa maeneo ya Ukraine. Nchi saba zilizopinga azimio hilo ni pamoja na Belarus, Nicaragua, Urusi, Syria, Korea Kaskazini, Eritrea na Mali ambazo zimeongeza ushirika wa kijeshi na Urusi.

Kura hiyo hata hivyo ilikuwa chini kidogo ukilinganisha na maazimio mengine matano yaliyopita ambayo yameidhinishwa na wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa tangu Urusi ilipotuma vikosi vyake na vifaru katika mpaka wa jirani yake mnamo Februari 24 mwaka 2022.

Russlands UN-Botschafter Wassili Nebensja in der UN-Vollversammlung
Mwakilishi wa kudumu wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vasily NebenzyaPicha: Michael M. Santiago/Getty Images

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell aliwaeleza waandishi wa habari kwamba mvamizi na muhanga hawawezi kuwekwa chini ya masharti sawa. Lakini naibu balozi wa China katika Umoja wa Mataifa Dai Bing kwa upande wake alisema kuwa wanaunga mkono Urusi na Ukraine kufanya mazungumzo na kwamba "jumuiya ya kimataifa inapaswa kufanya juhudi za kuwezesha mazungumzo ya amani".

"Mwaka mmoja katika mgogoro wa Ukraine, ukweli mchungu unatoa uthibitisho wa kutosha kwamba kutuma silaha hakutaleta amani. Kuongeza mafuta kwenye moto kutaongeza mvutano tu. Kurefusha na kupanua mzozo kutawafanya watu wa kawaida kulipa gharama kubwa zaidi," alisema Naibu balozi wa China katika Umoja wa Mataifa.Umoja wa Mataifa waamuru Urusi iondoe vikosi vyake Ukraine

China inadai kwamba haigemei upande wowote katika mzozo huo na inahimiza mazungumzo ya amani lakini haijakosoa uvamizi wa Urusi. Beijing imeikosoa Marekani na washirika wake kwa vikwazo dhidi ya Moscow na usaidizi wa kijeshi kwa Ukraine.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limekuwa chombo muhimu kinachoshughulikia mzozo wa Ukraine kwasababu baraza la usalama ambalo lina mamlaka ya kulinda usalama na amani ya kimataifa, limedhoofishwa na kura ya turufu ya Urusi. Ingawa maamzimio ya Baraza kuu hayana mamlaka kisheria tofauti na yale ya Baraza la Usalama lakini yanatumika kama kipimo cha maoni ya ulimwengu.