Je, meli za kivita za EU zitawazuwia waasi wa Houthi?
23 Januari 2024Huku makombora yakifyatuliwa katika Bahari ya Shamu kati ya Marekani kwa ushirikiano wa Uingereza na waasi wa Kihouthi wa Yemen, Umoja wa Ulaya unapanga jibu lake dhidi ya mgogoro huo mpya ambao uko mbali na mpaka wa Israeli na Palestina, lakini umefungamana na mzozo wa Gaza.
Umoja wa Ulaya unaanzisha dhamira mpya ya kulinda meli baharini pamoja na maslahi ya umoja huo kibiashara katika eneo hilo muhimu kimkakati. Lakini wachambuzi wametahadharisha kuwa hatari ya kuongezeka kwa mzozo wakati wa jitihada za kuwazuia Wahouthi ni kubwa. Hivyo basi ni lazima Umoja wa Ulaya uchukue tahadhari kubwa.
Ni kwa nini EU inazingatia misheni ya Bahari Nyekundu?
Kwa wiki kadhaa sasa Wahouthi wanaodhibiti maeneo makubwa ya kaskazini na magharibi mwa Yemen, wamekuwa wakizishambulia meli za kibishara katika Bahari ya Shamu, moja kati ya njia yenye usafiri na uchukuzi mwingi wa kibiashara duniani, ikiunganisha Bahari ya Arabia na Bahari ya Mediterania kupitia Mfereji wa Suez.
Kundi hilo linalotajwa kuwa la kigaidi na linaloshirikiana na Iran, lilianzisha mashambulizi yake kufuatia operesheni ya kijeshi ya Israel katika Gaza, operesheni iliyochochewa na shambulizi la kigaidi la Oktoba 7 dhidi ya Israel, lililofanywa na kundi la Hamas. Israel, Marekani, Umoja wa Ulaya miongoni mwa nchi nyingine zimeliorodhesha kundi la Hamas kuwa kundi la kigaidi.
Soma pia: Wahouthi wazishambulia meli za Marekani kwa droni
Wahouthi wanasema mashambulizi yao ni ishara ya mshikamano wao na Wapalestina wanaoshambuliwa na Israel, na kwamba wanalenga meli ambazo zinahusiana moja kwa moja au kwa njia nyingine na Israel.
Kwa muda mrefu, Umoja wa Ulaya na madola mengine makubwa duniani wamekuwa wakilaani mashambulizi dhidi ya meli na kusema ni uhalifu. Takriban asilimia 40 ya biashara zote kati ya Ulaya, Asia na Mashariki ya Kati hupitia Bahari ya Shamu. Meli nyingi zimelazimika kuchukua njia ndefu inayozunguka Afrika, hali inayochelewesha biashara na kusababisha hasara zaidi.
Mpango wa Umoja wa Ulaya ambao hata hivyo haujafikiwa, na ambao huenda pia ukachukua wiki kadhaa kabla ya kukamilishwa, utakuwa tofauti na Operesheni ya Ulinzi ya Washington. Operesheni hiyo imezijumuisha takriban nchi 20
Je mpango wa EU ukoje?
Mapendekezo kadhaa yametolewa lakini wazo kuu ni kupeleka meli za kivita na manowari kushika doria katika eneo hilo.
Huduma ya Utekelezaji ya Nje ya Ulaya, ambayo ni huduma ya kidiplomasia ya kigeni ya Umoja wa Ulaya ilipendekeza kutuma angalau meli tatu za kivita. Hiyo ni kulingana na vyombo vingi vya habari vinavyotaja hati ya ndani iliyovuja ya umoja huo.
Kulingana na mwanadiplomasia aliyezungumza na DW kwa sharti la kutotambulishwa, baada ya mashauriano ya awali, pendekezo linaloungwa mkono ni kushirikisha operesheni iliyopo, Agenor, inayoongozwa na Ufaransa, ambayo inafuatilia matukio karibu na Mlango-Bahari wa Hormuz.
Soma pia: Waasi wa Houthi wasema wataanza kuzilenga meli za Marekani
Nchi nane za Umoja wa Ulaya tayari zinashiriki operesheni hiyo kama sehemu ya misheni pana kwa jina Uhamasishaji wa Usafiri wa Bahari wa Ulaya katika Mlango-Bahari wa Hormuz, (EMASoH), ambao "unanuia kutuliza mivutano na kuchangia katika mazingira salama ya usafiri baharini. Hiyo ni kulingana na tovuti ya misheni hiyo.
Umoja wa Ulaya unalenga kuwa na ujumbe ifikapo Februari 19, na kufanya kazi hivi karibuni. Shirika la habari la Reuters liliripoti hayo, likinukuu vyanzo vya kidiplomasia ambavyo havikutajwa. Kwa sasa, hatua inayofuata ni mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya siku ya Jumatatu.
Hatari zilizopo ni zipi?
Kulingana na mkurugenzi wa Taasisi ya Masuala ya Kimataifa ya Italia (IAI) Nathalie Tocci, miongoni mwa hatari zilizopo ni pamoja na meli za Umoja wa Ulaya kushambuliwa, na vilevile hatari kwamba mpango huo ukose kutimiza lililokusudiwa na kuufanya umoja huo kuonekana dhaifu.
Lakini kulingana na Camille Lons, mchambuzi kutoka Baraza la Ulaya la Mahusiano ya Kigeni (ECFR), ni muhimu kwa Umoja wa Ulaya kupata, "jibu dhidi ya vitisho vya usalama baharini ambavyo tunaona, kwa sababu vinalenga moja kwa moja usalama wao wa kiuchumi na maslahi.