Baerbock ataka kuipiga jeki Ukraine akiwa ziarani Kyiv
4 Novemba 2024Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema Ukraine inahitaji msaada wa kuiwezesha kuvuuka salama msimu mwingine wa baridi ikiwa vitani katikati ya uharibifu mkubwa wa miundombinu uliofanywa na mashambulizi ya majeshi ya Urusi.
Mwanadiplomasia huyo ametoa matamshi hayo baada ya kuwasili mjini Kyiv leo Jumatatu kwa ziara yake ya nane ya kuonesha mshikamano na Ukraine.
Soma pia: Zelensky asema serikali yake inahitaji "nguvu mpya"
Baerbock amesema Ukraine inapigania demokrasia na uhuru wa watu wote wa Ulaya na mataifa washirika yanapambana kuisaidia nchi hiyo kuvuka kipindi kigumu inachopitia.
Akiwa mjini Kyiv, Baerbock anatazamiwa kukutana na Rais Volodymyr Zelensky na waziri mwenzake wa nchi hiyo, Andrii Sybiha.
Ziara yake inafanyika wakati jeshi la Ukraine limesema mapema leo kwamba limedunguwa droni 50 kati ya 80 zilizorushwa na Urusi hali inayoashiria mapambano bado ni makali kwenye uwanja wa vita.