1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNigeria

Baada ya kushinda urais, Tinubu ahimiza mshikamano

Sylvia Mwehozi
1 Machi 2023

Rais mpya mteule wa Nigeria Bola Tinubu kutoka chama cha APC ametetea uadilifu wa tume huru ya taifa ya uchaguzi na kutoa wito wa mshikamano huku vyama vya upinzani vikitaja kasoro katika uchaguzi huo.

https://p.dw.com/p/4O6TR
Nigeria | Wahlen Bola Tinubu
Picha: Ben Curtis/AP Photo/picture alliance

"Tinubu Bola Ahmed wa APC, baada ya kukidhi matakwa ya kisheria, anatangazwa mshindi na kuandikwa kuwa rais mteule. Asante."

Ni tangazo la mwenyekiti wa tume huru ya taifa ya uchaguzi ya Nigeria INEC Mahmood Yakubu, juu ya matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyokuwa yakisubiriwa kwa shauku kubwa.

Tinubu amejizolea jumla ya kura milioni 8.79 katika uchaguzi uliofanyika mwishoni mwa Juma akiwa mbele ya mpinzani wake mkuu Atiku Abubakar aliyepata kura milioni 6.98. Peter Obi mgombea aliyepata umaarufu miongoni mwa vijana, wasomi na wapiga kura wa mijini ameibuka nafasi ya tatu na kura milioni 6.1.

Kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi, mgombea anaweza kushinda uchaguzi wa Nigeria kwa kupata kura zaidi kuliko wapinzani wake, mradi tu ashinde asilimia  25 ya kura angalau katika theluthi mbili ya majimbo 36 na mji mkuu wa shirikisho Abuja. Mara baada ya kutangazwa mshindi Tinubu amewaeleza wafuasi wake kwamba amekabidhiwa "majukumu makubwa" na anayakubali.

Nigeria I Atiku Abubakar
Mgombea Atiku Abubakar aliyeibuka nafasi ya pili katika kinyang'anyiro cha urais nchini Nigeria 2023Picha: Afolabi Sotunde/File Photo/File Photo/REUTERS

"Ni nchi moja ambayo lazima tuijenge pamoja. Tunafanya kazi pamoja ili kuziba ufa uliojitokeza. Lazima tufanye kazi kwa ajili ya umoja, furaha na maelewano. Naahidi nitashirikiana nanyi kuifanya Nigeria kuwa nchi ya kurejea nyumbani ili kuchangia maendeleo ya nchi, " alisema Tinubu.

Uchaguzi wa Nigeria ulikuwa unatazamwa kuwa wa haki na wa wazi, lakini mchakato huo uligubikwa na hitilafu kadhaa haswa kutokana na teknolojia mpya ambayo haikufanya kazi kama ilivyotarajiwa.Tinubu akaribia kupata ushindi wa uchaguzi nchini Nigeria

Tume ya uchaguzi ilikuwa imeahidi kwamba ingechapisha matokeo kutoka kila kituo cha kupigia kura kwenye tovuti yake kwa muda unaofaa, lakini vituo vingi vilishindwa kufanya hivyo kwa haraka na hivyo kutia dosari mchakato wenyewe.

Nigeria Wahlen 2023/Präsidentschaftskandidat Peter Obi
Peter Obi ni mgombea aliyeibuka nafasi ya tatu katika uchaguzi wa rais wa Nigeria 2023.Picha: Shengolpixs/IMAGO

Sababu hizo ndio zimechangia vyama vikuu vya upinzani vya Atiku na Obi kuyakataa matokeo wakidai kwa kuna udanganyifu. Rais mteule Tinubu sasa anakabiliwa na mlolongo wa matatizo kadha yanayolikumba taifa hilo, ikiwa ni pamoja na uasi wa wanamgambo wa Kiislamu wenye itikadi kali upande wa Kaskazini Mashariki, mashambulizi, mauaji, utekaji nyara, mzozo baina ya wafugaji na wakulima, uhaba wa mafuta, pesa taslimu na umeme pamoja na rushwa iliyokita mizizi.

Waangalizi wa kimataifa, wakiwemo kutoka Umoja wa Ulaya nao walibaini matatizo makubwa ya vifaa, wapiga kura kunyimwa haki na ukosefu wa uwazi wa tume ya uchaguzi INEC.Matokeo ya mwanzo katika uchaguzi wa Nigeria yaonesha Tinubu anaongoza

Rais anayemaliza muda wake Muhammadu Buhari pia kutoka chama cha APC amempongeza mrithi wake akisema kuwa "ni mtu sahihi kwa kazi hiyo" na yuko tayari kufanya kazi pamoja ili kukabidhi madaraka kwa amani.

Tinubu mwenye umri wa miaka 70 na mwanasiasa mkongwe, alijipambanua kwa kauli mbiu iliyosema "ni zamu yangu" na ameahidi kurejesha matumaini lakini amekabiliwa na maswali magumu kutoka kwa wapinzani juu ya afya yake, madai yaliyopita ya ubadhirifu na usuhuba wake na Buhari ambaye wakosoaji wengi wanadai kuwa ameshindwa kutimiza ahadi yake ya kudumisha usalama Nigeria.