Awamu ya pili ya kuondoa walinda amani Mali "itakuwa ngumu"
29 Agosti 2023Mkuu wa MINUSMA El-Ghassim Wane amesema awamu ya pili ya kuwaondoa walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaohudumu nchini humo itakumbwa na changamozo nyingi kutokana na muda uliosalia kuwa mchache na hali mbaya ya kiusalama.
Wane amesema kufikia Septemba 30, karibu theluthi moja ya wafanyikazi wa MINUSMA watakuwa wameondoka nchini Mali huku awamu ya pili itakayodumu hadi Disemba 15, ikihusisha wanajeshi hao kuziacha kambi sita upande wa kaskazini, kaskazini mashariki na katikati mwa Mali.
Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, unaojulikana kama MINUSMA, una hadi Disemba 31 kuondoka nchini Mali baada ya muongo mmoja wa kujaribu kuleta utulivu na kuimarisha usalama katikati ya uasi wa itikadi kali na mashambulizi kutoka makundi ya wanamgambo.
Ujumbe huo wenye askari 13,000 uliamriwa kufungasha virago mapema mwaka huu na utawala wa kijeshi wa Mali, kufuatia kuondoka kwa wanajeshi wa Ufaransa mnamo mwaka 2022.