Angola: MPLA yatangazwa mshindi, UNITA yakataa matokeo
27 Agosti 2022Kulingana na tume ya uchaguzi, chama hiki kilipata asilimia 44.5, ikiwa ni baada ya asilimia 97 ya kura zote kuhesabiwa siku ya Alhamisi.
Msemaji wa chama cha MPLA Rui Falcao aliuambia mkutano wa waandishi wa habari mjini Luanda jana jioni, kuwa kwa mara nyingine chama chao kimepata ushindi wa kutosha kuweza kuiongoza nchi bila matatizo yoyote. Hata hivyo, chama cha upinzani cha UNITA kilipata ushindi wa kishindo katika mji huo mkuu.
Soma zaidi: Waangola kuamua kati ya Lourenco na Costa Junior
Kwa upande mwingine, mwenyekiti wa UNITA Costa Junior akizungumza na waandishi wa habari kwa mara ya kwanza tangu siku ya uchaguzi, alitupilia mbali alichokiita tofauti ya ''kikatili'' baina ya majumuisho yao ya kura na yale yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi.
Amesema hana shaka lolote kwamba MPLA haikupata ushindi, na kwa hivyo UNITA haiyatambui matokeo hayo ya awali.
MPLA chaonja joto la ushindani halisi
Huu ni uchaguzi wa kwanza wa Angola ambapo chama tawala kimepata ushindani mkubwa kutoka chama cha upinzani. Wachambuzi wanahofu kuwa ikiwa matokeo haya yatafuatiwa na ubishani, hali hiyo inaweza kusababisha vurugu kubwa miongoni mwa vijana masikini na waliokata tamaa, ambao wengi wao walikichagua chama cha UNITA.
Kiongozi wa chama hicho, Costa Junior amewataka vijana hao kuendelea kuwa watulivu, na kwa sehemu kubwa wameitikia wito huo wa amani, isipokuwa tu visa vichache vya maandamano ambayo yalitawanywa na polisi kwa virungu na gesi ya kuwasha machoni.
Soma zaidi: Ushindani mkali watarajiwa katika uchaguzi wa Angola
Asasi zisizo za kiserikali zilichapisha vidio mitandaoni zilizoyaonyesha makundi ya vijana waliobeba mabango, wakitembea na kuimba nyimbo za kupinga udanganyifu katika uchaguzi. Hata hivyo, shirika la reuters lililoripoti tukio hilo, halikuweza kuthibitisha uhalisia wa picha hizo.
Hata hivyo, njia halali aliyo nayo kisheria kiongozi huyo wa UNITA ni kupeleka malalamiko yake katika tume ya uchaguzi, na ikiwa yatakataliwa, atasaliwa na chaguo la kuiendea mahakama ya katiba, ambayo inapashwa kubainisha uamuzi wake katika muda wa saa 72.
Malalamiko ya UNITA kuishia mahakamani?
Ikiwa matokeo yatabaki kama yalivyo, itakuwa mara ya kwanza kwa UNITA kuipokonya MPLA theluthi mbili ya viti bungeni, ambayo inahitajika kupitisha maamuzi magumu.
Lakini pengine kitu cha kushangaza zaidi ni namna uchaguzi huu wenye ushindani mkubwa kati ya vyama viwili vilivyohodhi siasa za Angola tangu ilipopata uhuru wake, ulivyoitiwa na idadi ndogo kabisa ya wapiga kura.
Soma zaidi: Rais wa zamani wa Angola José Eduardo Santos afariki dunia
Takwimu za uchaguzi zilizochapishwa jana Ijumaa, zimeonyesha kuwa ni asilimia 45.65 tu ya watu wenye sifa ya kupiga kura waliojitokeza kufanya hivyo.
Rais wa sasa, Joao Lourenco ameahidi kuendeleza sera yake ya mabadiliko, inayojumuisha kubinafsisha mashirika ya serikali yanayoendeshwa kwa hasara.
Hata hivyo, raia wengi wa Angola bado wanaishi katika lindi la umaskini, licha ya ahadi za muda mrefu za kugawanya kwa usawa zaidi utajiri wa taifa hilo ambalo ni la pili kwa kuzalisha mafuta barani Afrika.
-afpe, rtre