Waangola kuamua kati ya Lourenco na Costa Junior
24 Agosti 2022Wananchi wa Angola leo wamejitokeza kwenye vituo vya kupigia kura katika uchaguzi wa rais unaotarajiwa kuwa na ushindani mkali kati ya mgombea wa chama tawala cha MPLA na yule wa upinzani kutoka chama cha UNITA.
Wapiga kura nchini Angola walijitokeza tangu mapema kabisa asubuhi kwenye vituo vya kupigia kura kumchagua rais mpya katika uchaguzi ambao vyama vinane vimeweka wagombea wao katika kinyang'anyiro hicho cha urais. Hata hivyo inaelezwa kwamba mchuano mkali utakuwa ni kati ya wagombea wawili rais wa sasa anayetetea nafasi yake Joao Lourenco na kiongozi wa upinzani Adalberto Costa Junior.
Masuala makubwa yanayoamua uchaguzi huu ni uchumi uliozorota,ughali wa maisha,kuongezeka kwa umasikini kulikosababishwa na janga la Corona,ukame katika baadhi ya maeneo ya Kusini mwa nchi hiyo pamoja na kifo cha rais wa zamani aliyekuwa na sauti nchini humo Jose Eduardo Dos Santos atakayezikwa Jumapili.
Rais wa sasa Lourenco alipiga kura yake mapema kabisa hii leo kwenye kituo kilichokuwa na ulinzi mkali na kisha akawatolea mwito waangola wajitokeze kutimiza haki yao ya kikatiba kama alivyofanya yeye na kusisitiza kwamba demokrasia itashinda nchini humo. Kiasi watu milioni 14.7 wamejiandikisha kupiga kura kukiwa na vituo 13,200 vya kupigia kura kote nchini humo.
Kadhalika kwa mara ya kwanza Waangola wanaishi nje walipewa nafasi ya kushiriki zoezi hilo.Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa moja kamili asubuhi na vitafungwa saa kumi na moja kamili jioni hii. Taasisi ya kimataifa inayojihusisha na masuala ya siasa- Eurasia group imeashiria kwamba ikiwa waangola watajitokeza kwa wingi kupiga kura basi chama tawala cha MPLA kinatarajiwa kupata ushindi ingawa ikiwa itatokea kinyume chake basi chama cha upinzani UNITA kitakuwa kwenye nafasi nzuri ya kunyakua ushindi.
Chama tawala ambacho kimeshikilia madaraka kwa takriban miongo mitano kinakabiliwa na upinzani mkali sana mara hii ikiwa ni kwa mara ya kwanza tangu nchi hiyo ilipofanya uchaguzi uliovishirikisha vyama vingi mnamo mwaka 1992. Mchambuzi wa kisiasa Joao Gomes Goncalves anasema.
"Changamoto ni nyingi,tuna changamoto ya kuleta uthabiti nchini,tuna tatizo la rushwa,tuna tatizo la uchumi tuna matatizo ya kijamii,kwahivyo chama kitakachoshinda uchaguzi huu kitakuwa na changamoto nyingi zinazowasubiri,changamoto nyingi ambazo hata sijamaliza kuziorodhesha hapa.Kwasababu nchi yetu kama nchi nyingine zinazoitwa hazijaendelea,ni nchi ambayo pia imetikishwa na janga la Corona.''
Kuna wagombea wa vyama vinane kwa ujumla wanaowania kiti hicho cha urais na kura za maoni zilizochapishwa mara ya mwisho hivi karibuni zimeonesha kwamba uungwaji mkono wa chama tawala MPLA ambacho kilijizolea asilimia 61 ya kura katika uchaguzi wa mwaka 2017 utapungua wakati chama cha waasi wa zamani cha UNITA ambacho kimeungana na vyama vingine viwili kitajiongezea umaarufu.
Matokeo ya uchaguzi huu yanatarajiwa kutangazwa ndani ya siku chache zijazo ingawa chaguzi za huko nyuma zimeonesha uzoefu kwamba mara nyingi matokeo hupingwa kupitia mchakato ambao unaweza kuchukua wiki chungunzima.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri: Daniel Gakuba