Amnesty yaonya kuhusu kuongezeka kwa tofauti za kidunia
26 Februari 2019Ripoti iliyotolewa na shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International imeonya kuhusu kuwepo kwa tofauti za kidunia kuelekea masuala ya haki za binaadamu zinachochea kuongezeka kwa ukiukwaji mkubwa wa haki hizo katika maeneo ya Mashariki ya Kati na Magharibi mwa Afrika ambao ulifanywa na serikali.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya mwaka ya shirika hilo katika kanda ya Mashariki ya Kati iliyotolewa Jumanne (26.02.2019) mjini Beirut ukandamizaji kwa wanaharakati wa mashirika ya kiraia na wanasiasa wa upinzani vimeongezeka kwa kiasi kikubwa nchini Misri, Iran na Saudi Arabia.
Imeangazia pia mauaji yaliyofanywa na maafisa wa kijasusi wa Saudi Arabia dhidi ya mwandishi habari Jamal Khashoggi katika ubalozi mdogo wa taifa hilo la kifalme, mjini Instanbul, Uturuki mnamo mwezi Oktoba likisema hakukuwa na hatua yoyote thabiti iliyofuatia kutokana na mauaji hayo ili kuhakikisha wahusika wanatiwa nguvuni.
Amnesty International imesema mauaji ya Khashoggi yalichochea kuchukuliwa kwa hatua za nadra kutoka nchi kama Denmark na Finland za kusimamisha biashara ya silaha kwa Saudi Arabia.
Imeongeza kuwa washirika muhimu wa saudi Arabia, ambao ni pamoja na Marekani, Uingereza na Ufaransa hawakuchukua hatua yoyote kama hiyo na kwa ujumla jamii ya kimataifa imeshindwa kufikia matakwa ya mashirika ya kimataifa haki za binaadamu ya kutaka Umoja wa Mataifa kufanya uchunguzi huru utakaowezesha kupatikana kwa haki.
Kuhusu mzozo wa Yemen, shirika hilo limetoa mwito kwa mataifa yote kusitisha mara moja mauzo ya silaha kwa Israel na pande zinazovutana nchini Yemen hadi pale silaha hizo zitakapoonekana kuwa sio kitisho tena na kutumika katika matukio ya ukiukwaji wa haki za binaadamu.
Mzozo wa Yemen ulianza mwaka 2014 baada ya kuchukuliwa kwa mji mkuu Sanaa, na wanamgambo wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran na walioangusha serikali ya Abed Rabbo Mavsour Hadi. Vita hivyo vimesababisha vifo vya maelfu ya raia huku wengine mamilioni wakikabiliwa na kitisho cha baa la njaa na upungufu wa dawa.
Amnesty iliuchukulia mwaka 2018 kama mwaka wa aibu kwa Iran kulingana na ripoti hiyo kufuatia mamlaka kuwakamata zaidi ya waandamanaji 7,000, wanafunzi, waandishi wa habari na wengine ambao wengi wao ni wapinzani.
Nchi Saudi Arabia, mamlaka ziliwatia nguvuni na kuwafungulia mashitaka wakosoaji wa serikali, wasomi na watetezi wa haki za binaadamu. Kwenye wimbi la kamata kamata hiyo mnamo mwezi Mei 2018 takriban wanawake wanane watetezi wa haki za binaadamu waliofanya kampeni dhidi ya zuio la wanawake kuendesha magari na mfumo dume walitiwa kizuizini bila ya kufunguliwa mashitaka.
Nchini Misri hali ilikuwa mbaya zaidi hasa baada ya kukamatwa wagombea wa tiketi ya urais kutoka upinzani.
Mwandishi: Lilian Mtono/APE
Mhariri: Sekione Kitojo