Amnesty: Wanaorudi Syria wanateswa na kubakwa
7 Septemba 2021Kwenye ripoti yake yenye kichwa ‘Unakiendea Kifo Chako', shirika la Amnesty International limeorodhesha mateso yaliyofanywa na maafisa wa usalama ikiwa ni visa 66 vya Wasyria miongoni mwao watoto 13 waliorudi nchini humo tangu mwaka 2017. Amnesty imetahadharisha ikisema hakuna sehemu ambayo ni salama nchini Syria kwa watu kurudishwa.
Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limesema maafisa wa ujasusi wa Syria huwaweka kizuizini wanawake na watoto wanaorudi nchini humo kinyume cha sheria, kuwatesa, ubakaji, dhuluma nyinginezo za kingono na watu kutoweka kwa njia ya kutatanisha.
Miongoni mwa visa vilivyoorodheshwa, Amnesty ilinakili visa vitano vya watu waliokufia kizuizini baada ya kurudi Syria. Shirika hilo limesema hatima ya watu wengine 17 waliotoweka kwa njia ya kutatanisha bado haijulikani.
Manyanyaso mikononi mwa maafisa wa usalama
Aidha, shirika hilo lilinakili visa 14 vya manyanyaso ya kingono yaliyofanywa na maafisa wa usalama ikiwa ni pamoja na visa saba vya ubakaji dhidi ya wanawake watano, ulawiti dhidi ya mvulana mmoja na msichana wa miaka mitano aliyenajisiwa.
Soma pia Umoja wa Mataifa waongeza muda wa misaada Syria
"Serikali yoyote inayodai kwamba Syria ni salama, inapuuza kwa hiari yake mwenyewe hali halisi ya kushtusha iliyoko nchini humo,” shirika la Amnesty limesema.
Zaidi ya watu milioni 6.6 raia wa Syria wamekiimbilia nchi yao tangu machafuko yalipoanza nchini humo mwaka 2011, wengi wao wakiwa katika nchi jirani mathalan Uturuki au Lebanon.
Shinikizo kutaka wakimbizi wa Syria kurudi nchini mwao
Kwa mujibu wa Amnesty katika siku za hivi karibuni, Denmark, Sweden na Uturuki zimekuwa zikiongeza shinikizo kutaka wahamiaji wa Syria kurudishwa nchini mwao zikidai nchi hiyo sasa ni salama.
Raia waliohojiwa na Amnesty International ni pamoja na wahamiaji waliorudi Syria kutoka Lebanon, taifa ambalo limezidisha shinikizo kutaka wakimbizi hao kurudi Syria.
Soma pia: UN: Syria inahitaji misaada ya kibinadamu
Ripoti hiyo iliangazia pia ushuhuda uliotolewa na mwanamke mmoja kwa jina Alaa, aliyekamatwa pamoja na bintiye mwenye umri wa miaka 25 wakivuka mpaka kutoka Lebanon, wakawekwa kuzuizini kwa siku tano.
Mama huyo alisimulia kwamba maafisa walimvua bintiye nguo, wakamfunga pingu, wakamtundika ukutani na kumpiga akiwa uchi wa mnyama na kumnyanyasa kingono. Ripoti hiyo ilimnukuu Alaa akisema hayo.
(AFPE)