Amnesty yamshutumu Ndayishimiye kwa ukiukaji wa haki
20 Agosti 2024Ripoti hiyo imebainisha kuwa kipindi hicho kimetawaliwa na vitendo vya ukiukaji wa haki vikiwemo unyanyasaji, watu kukamatwa kiholela, mashtaka yasiyo ya haki pamoja na vitisho.
Taarifa ya Amnesty International imebainisha kwamba miongoni mwa waliokabiliwa zaidi na ukandamizaji huo wa haki ni watetezi wa haki za binadamu, wanaharakati, waandishi wa habari na wanachama wa vyama vya upinzani.
Akizungumza wakati wa kutoa ripoti hiyo, Mkurugenzi wa shirika hilo katika kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika Tigere Chagutah, ameeleza kuwa, wimbi hilo la uonevu linaloendelea, limefifisha matumaini ya mabadiliko yenye manufaa kwa asasi za kiraia na nafasi ya mjadala kuhusu masuala yanayohusu haki za binadamu nchini humo.
Soma zaidi: Marekani yaitaka Burundi kuheshimu haki za binaadamu
Kulingana na ripoti hiyo, baada ya maandamano makubwa ya mwaka 2015 na jaribio la mapinduzi ya kijeshi, serikali ya rais wa zamani wa Burundi Pierre Nkurunziza, ilichukua hatua kali zilizosababisha moja ya asasi mahiri za kiraia nchini humo kushindwa kuendelea na shughuli zake kama hapo awali.
Amnesty International imeongeza kuwa, baada ya Rais Ndayishimiye kuingia madarakani kulikuwa na matumaini kuwa angelegeza msimamo wa serikali dhidi ya asasi za kiraia na vyombo vya habari baada ya kuachiliwa huru kwa watetezi wawili wa haki za binadamu na waandishi wanne wa habari. Watu hao wote waliokuwa wamehukumiwa kifungo jela kutokana na kazi zao waliachiliwa huru katika mwaka wa kwanza wa Ndayishimiye madarakani.
Kamata kamata kiholela bado inaendelea Burundi
Hata hivyo utafiti wa shirika la Amnesty International umeonesha kuwa, licha ya kuwa watetezi wa haki za binadamu waliokamatwa kabla ya Rais huyo kuingia madarakani waliachiliwa huru, wengine walikamatwa kiholela na kushtakiwa kwa tuhuma zinazofanana na za walioachiliwa.
Ripoti hiyo ilitolewa baada ya mahojiano na watu wanaofahamu kuhusu mikasa iliyotajwa, nyaraka za kisheria,, ripoti za vyombo vya habari na hotuba rasmi. Imeainisha mifano kadhaa ya ukamatwaji kiholela likiwemo tukio la, Oktoba 2022 alipokamatwa mwanasheria Tony Germain Nkina kutokana na shughuli zake za kipindi cha nyuma za kutetea haki za binadamu.
Soma zaidi: Ripoti mpya yabainisha matukio ya mateso na mauwaji Burundi
Amnesty International limetoa wito kwa Rais Ndayishimiye na serikali yake kukomesha ukandamizaji wakati nchi hiyo ikielekea katika uchaguzi wa bunge uliopangwa kufanyika mwakani. Limeongeza kuwa, mamlaka za Burundi zinapaswa kuacha haraka kuwakamata watu ovyo, na kuwashtaki watetezi wa haki za binadamu.
Zaidi limeitaka Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kuutathmini mwenendo wa Burundi katika ahadi yake ya kuboresha heshima kwa haki za binadamu na kuzishirikisha asasi za kiraia nchini humo katika kuhakikisha uwajibikaji.