Algeria yawakamata watu saba kwa tuhuma za ujasusi
2 Septemba 2024Algeria imesema imewatia mbaroni watu saba wakiwemo Wamorocco wanne wanaotuhumiwa kwa kuwa wanachama wa mtandao wa ujasusi.
Hayo yamesemwa na waendesha mashitaka wa Algeria siku ya Jumapili, chini ya wiki moja kabla uchaguzi wa rais kufanyika nchini humo.
Maafisa katika mji wa kaskazini magharibi wa Tlemcen, karibu na mpaka wa Morocco wamesema watu hao waliotiwa mbaroni wamewekwa katika kizuizi cha muda kufuatia kusambaratishwa kwa mtandao wa ujasusi uliolenga kuvuruga usalama wa dola.
Waendesha mashitaka wamesema uchunguzi wa mahakama umeanzishwa kuhusu madai yakiwemo ya kufanya ujasusi kwa ajili ya nchi nyingine, huku raia watatu wa Morocco pia wakishukiwa kwa kuingia Algeria kinyume na sheria.
Algeria itafanya uchaguzi Jumamosi ijayo kumchagua rais. Rais wa sasa Abdelmadjid Tebboune anapewa nafasi kubwa kumshinda mwanasiasa mwenye msimamo wa wastani Abdelaali Hassani na msoshalisti Youssef Aouchiche.