1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAlbania

Albania yaidhinisha mkataba wa kuwahifadhi wahamiaji

22 Februari 2024

Bunge la Albania limeiidhinisha mkataba wenye utata uliotiwa saini kati ya nchi hiyo na Italia wa kuwahifadhi wahamiaji waliookolewa katika eneo la maji la Italia.

https://p.dw.com/p/4ckt7
Bunge la Albania
Waziri Mkuu wa Albania Edi Rama akizungumza wakati wa mjadala katika bunge la Tirana, Albania.Picha: Franc Zhurda/AP Photo/picture alliance

Makubaliano hayo, ambayo yalihitaji wingi mdogo tu wa kura, yalipitishwa kwa kuungwa mkono na wabunge 77 wa bunge hilo lenye viti 140, huku upinzani ukisusia kura hiyo.

"Albania inasimama pamoja na Italia kwa kuchagua kufanya uamuzi kana kwamba ni nchi mwanachama waUmoja wa Ulaya," Waziri Mkuu Edi Rama alisema katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii.

Alisema Albania inasaidia "kushiriki kubeba mzigo ambao Ulaya inapaswa kukabiliana nao kwa umoja kama familia chini ya kitisho cha migawanyiko inayoshuhudiwa pande zote za siasa (kwa maana ya wale) wa mrengo wa kushoto na kulia".

Soma pia:Mahakama Italia yaharamisha kuwarejesha wahamiaji Libya

Makubaliano hayo yamekuwa yakikashifiwa mara kwa mara na vyama vya upinzani katika nchi zote mbili na pia mashirika ya haki, na kusababisha pingamizi la kisheria lililowasilishwa kwenye mahakama ya juu ya Albania huko mjini Tirana.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, mahakama hiyo ya kikatiba iliidhinisha mpango huo, na kufungua njia ya kura ya kuuridhia mkataba huo.

 

Athari za Mkataba huo

Albania
Waandamanaji katika Mahakama ya Katiba, wakipinga makubaliano ya Italia na Albania kuhusu wahamiaji.Picha: Rashela Shehu

Upinzani wa Albania umekosoa makubaliano hayo. "Mkataba wa wahamiaji unadhuru usalama wa taifa, uadilifu wa eneo na maslahi ya umma," kiongozi wa upinzani wa mrengo wa kulia Gazmend Bardhi aliwaambia waandishi wa habari.

Uidhinishaji huo wa bunge umejiri wiki kadhaa baada ya wabunge wa Italia pia kupiga kura ya kuunga mkono mpango huo, huku Baraza la Wawakilishi la Bunge likiunga mkono kwa kura 155 dhidi ya 115, na  wabunge wawili wakijizuia kushiki katika zoezi hilo.

Soma pia: Italia haijatimiza malengo ya kudhibiti wahamiaji

Makubaliano hayo yanaruhusu kujengwa kwa vituo viwili karibu na bandari ya Albania ya Shengjin, ambapo wahamiaji watajiandikisha kupata hifadhi, pamoja na kituo kingine katika eneo hilo hilo cha kuwahifadhi wale wanaosubiri majibu ya maombi yao.

Vituo hivyo, vitakavyosimamiwa na Italia, vitaweza kuwahudumia watu wasiozidi 3,000 kwa wakati mmoja wakati wakisubiri uamuzi wa kesi zao.

Shirika lisilo la kiserikali la International Rescue Committee pia limelaani makubaliano hayo na kuyataja kama "ya kudhalilisha utu", huku Amnesty International ikiyataja kuwa "haramu na yasiyotekelezeka".

Mamlaka za Albania, hata hivyo, zimekaidi, zikisema kuwa mkataba huo unaendana na mikataba ya awali iliyotiwa saini na Italia, na unazingatia sheria za kimataifa na katiba ya nchi hiyo.

Fedha zitakazotumika

Giorgia Meloni
Waziri mkuu wa Italia Georgia Meloni aliahidi kukabiliana na ongezeko la wakimbizi.Picha: LUDOVIC MARIN/AFP/Getty Images

Kulingana na mamlaka ya Albania, Italia itafadhili ujenzi wa vituo hivyo viwili na miundombinu muhimu, pamoja na gharama zinazohusiana na usalama na matibabu ya wanaotafuta hifadhi.

Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni -- kiongozi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Ndugu wa Italia -- alichaguliwa kushika wadhifa huo mwaka 2022, ambapo aliahidi kusitisha boti za wahamiaji zinazowasili kutoka Afrika Kaskazini.

Lakini idadi ya waliowasili imeendelea kuongezeka, Takwimu rasmi zinaonyesha idadi imeongezeka kutoka watu 105,000 mwaka 2022 hadi kufikia karibu 158,000 mwaka jana.