Afrika Kusini yachungulia hatua ya mchujo
24 Januari 2013Wenyeji Afrika Kusini walipata ushindi wao wa kwanza tangu mwaka 2004 kwa kuifunga Angola magoli 2-0 katika uwanja wa Moses Mabhida mjini Durban na kukalia usukani wa kundi hilo wakiwa na jumla ya pointi nne.
Magoli kutoka kwa mlinzi Siyabonga Sangweni na Lehlohonolo Majoro yaliimpunguzia shinikizo kocha Gordon Igesund, wakati timu hiyo ilipoonyesha mchezo safi kuliko ule wa ufunguzi siku ya Jumamosi, ambapo Afrika Kusini ilitoka sare ya bila kufunguna na visiwa vya Cape Verde mjini Johannesburg. Igesund alifanya mabadiliko matano katika kikosi cha Jumamosi, na kusema kuwa alicheza kamari kwa kufanya mabadiliko mengi lakini kamari hiyo imelipa faida.
Morocco yanusurika kufedheheshwa
Visiwa vya Cape Verde, ambavyo ni taifa dogo la wakaazi laki tano tu, likishiriki fainali hizo kwa mara ya kwanza, liliingia katika dakika 12 za kile ambacho kingekuwa ushindi wake mkubwa zaidi wa kimichezo, lilipoingoza Morocco kwa goli 1-0 huku firimbi ya mwisho ikikaribia. Luis Soares alifunga goli la kwanza kabisaa la Cape Verde katika fainali hizo katika dakika ya 35, lakini Morocco ambayo ilishindwa kufungana na Angola katika mchezo wao wa kwanza, ilitawala mchezo huo baada ya mapumziko.
Hatimaye walifanikiwa kufuta uongozi wa Cape Verde katika dakika ya 78 wakati Youssef El Arabi alipozamisha mpira wavuni, kufuatia pasi maridhawa kutoka kwa Abdelazizi Barrada. Ingawa goli hilo liliikosesha Cape Verde kile ambacho kingekuwa fadhaa kubwa zaidi ya mashindano hayo, halikuwa zaidi ya kile ilichokihitaji Morocco, na liliacha kundi hilo likiwa limesawazishwa vizuri. Zikiwa chini ya Afrika Kusini, Cape verde na Morocco zote zina pointi mbili, huku Angola ikiwa mkiani kwa kuwa na pointi moja.
Baada ya ushindi wa magoli 2-0 tangu iliposhinda dhidi ya Benin miaka tisa iliyopita, Afrika Kusini sasa itakabiliana na Morocco katika mchezo wao wa mwisho wa hatua ya makundi mjini Durban siku ya Jumapili. Kwa upande wake Cape Verde itakutana na Angola mjini Port Elizabeth, katika pambano la makoloni mawili ya zamani ya Ureno. Timu zote nne zina nafasi ya kufuzu hatua ya mchujo na wadadisi wengi hawakudhani kama hilo lingetokea kabla ya kuanza kwa michuano hiyo, ambapo wengi waliichukulia Cape Verde kama timu isiyoweza licha ya ukweli kwamba iliiondoa Cameroon katika hatua ya kufuzu. Lakini sasa timu hiyo inapewa nafasi ya kushinda itakapokutana na Angola.
Ghana kulipiza kisasi kwa Mali leo?
Leo Alhamisi vinara wa kundi B Mali wanakabiliana na Ghana katika kile kinachoonekana kama marudio ya mchezo wa mwaka jana wa kuwania nafasi ya tatu na nne, ambapo Mali ilishinda 1-0. Baada ya sare katika mchezo wa kwanza, Ghana inakabiliwa na shinikizo kubwa, na nahodha wake Asamoa Gyan analifahamu hilo.
"Mimi ndiyo kiongozi mimi ndiyo nahodha, na uzoefu wowote niliyo nao, hivi sasa nautoa kwa wachezaji wachanga, na hicho ndicho nilichofanya baada ya mechi. Nadhani wachezi wengi ni wataalamu na tunajua uwezo wetu," alisema Asamoa.
Ghana hawajashinda kombe la mataifa ya Afrika tangu mwaka 1982. Wamefika hatua ya nusu fainali katika michuano mitatu iliyopita na kuna shinikizo kubwa kwao kufanikiwa mara hii.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre
Mhariri: Josephat Charo