AFCON 2013: Umdhanie sie kumbe ndie
23 Januari 2013Lakini Congo na Ethiopia zilikuja kutawala mazungumzo hayo kutokana na ujasiri walioonesha katika mashindano hayo.
Chui wa Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo waliweka kando manung'uniko yao kuhusu fedha za bonasi pamoja na unyanyasaji wanaotendewa na maafisa wa timu hiyo na kufuta kipigo cha mabao 2-0 na hatimaye kumaliza mchezo wao dhidi ya Ghana kwa sare ya mabao 2-2.
Ghana ilipewa nafasi ya juu
Ghana waliwekwa katika nafasi ya juu na Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo mwishoni kabisa katika kundi B na mchezo wao uliofanyika mjini Port Elizabeth ulionekana kuwa unakwenda katika mwelekeo wa utabiri huo, wakati Emmanuel Agyeman Badu na Kwadwo Asamoah walipopachika mabao ya Black Stars wa Ghana.
Lakini Chui hao wa msitu wa Virunga hawatabiriki na badala ya kusalimu amri, walifanikiwa kupata mabao mawili kutoka kwa nahodha wao, Tresor Mputu, na Dieumerci Mbokani alisawazisha kwa mkwaju wa penalti.
Mali inashikilia nafasi ya kwanza katika msimamo wa kundi B baada ya kuwalazimisha Niger kuacha ubishi zikiwa zimesalia dakika sita kabla mchezo kumalizika wakati golikipa, Daouda Kassaly, kujikuta hana hakika ya kuukamata mpira wa juu na kumzawadia Seydou Keita fursa adimu ya kupachika bao.
Ethiopia yarejea kwa kishindo
Ethiopia, ikirejea katika kinyang'anyiro cha kombe la mataifa ya Afrika baada ya ukame wa miaka 31, ilikosa penalti, na mlinda mlango wao Jemal Tassew alitolewa nje kwa kadi nyekundu na wakafungwa bao na mabingwa watetezi Zambia kabla ya kwenda mapumziko katika uwanja wa Nelspruit.
Lakini paa hao wa Walias walinakili yale yaliyofanywa na Chui wa Congo na kuweza kusawazisha bao hilo kwa gonga safi na kuuweka mpira wavuni wakimwacha golikipa wa Chipolopolo, Kennedy Mweene, akigaaga chini.
Burkina Faso na Nigeria nazo zina pointi moja kila mmoja katika kundi C. Togo iliwashangaza watabiri kwa kuiita timu isiyokuwa na matumaini katika timu 16 zilizofikia fainali, na ilibakisha tu dakika mbili kabla ya kuikaba koo Cote D'Ivoire katika kundi D, pale iliposalimu amri dakika za majeruhi na kukubali kipigo cha mabao 2-1. Lakini hata hivyo ilionyesha kandanda la ujasiri.
Leo ni zamu ya wenyeji Bafana Bafana, Afrika kusini kuonesha kuwa ni miongoni mwa timu zinazopigiwa upatu kutoroka na taji hilo, wakati itakapopambana na Angola. Wageni wa mashindano haya, Cape Verde, wakiwa katika hali sasa ya kujiamini wanatiana kifuani na Morocco.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Josephat Charo