Afrika katika magazeti ya Ujerumani
6 Oktoba 2017Kwa muda mrefu ni mambo matatu ambayo yamekuwa yanajitokeza mtu alipozungumzia juu ya Nigeria. Mambo hayo ni mafuta, ufisadi na Boko Haram. Mambo hayo matatu yanachanganyika katika kuathiri fursa za siku za usoni kwa nchi hiyo. Mafuta, bidhaa inayoiingizia Nigeria karibu asilimia 90 ya fedha za kigeni, yamepungua bei kwenye soko la dunia. Gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine linaeleza kwamba tangu kuangukua kwa bei ya mafuta, uchumi wa Nigeria umeshuka. Gazeti hilo linasema changamoto kubwa inayoikabili Nigeria ni kutafuta njia ya kupunguza kutegemea mafuta na kujaribu kuunyambua uchumi wake. Na ili kuwavutia wawekezaji vitega uchumi rais Muhammadu Buhari ameahidi kupambana vikali dhidi ya ufisadi na pia magaidi wa kundi la Boko Haram.
die tageszeitung
Gazeti la die tageszeitung linasema sehemu ya nchi hiyo inataka kujitenga, lakini serikali haitaki mchezo. Gazeti hilo linaeleza kuwa wanaharakati wa sehemu ya kusini mwa Cameroon iliyokuwa chini ya usimamizi wa wakoloni wa Uingereza wamejitangazia uhuru ili kujitenga na Cameroon inayotawaliwa na rais Paul Biya anayetokea sehemu ya watu wanaotumia lugha ya kifaransa. Serikali ya Rais Biya haikuchuchelewa kuchukua hatua madhubuti ili kuuzima uasi. Serikali hiyo iliufunga mpaka wake na Nigeria na kutangaza amri ya kutotoka nje. Mikutano ya watu zaidi ya wanne ilipigwa marufuku na usafiri baina ya miji mikubwa ulisimamishwa.
Gazeti hilo la die tageszeitung linakumbusha kwamba mnamo miaka ya 90 yalifanyika maandamano makubwa dhidi ya rais Paul Biya anayetawala Cameroon tangu mwaka wa1982. Watu wa kusini mwa Cameroon waliokuwa chini ya utawala wa Waingereza wanasema wanakandamizwa na serikali kuu inayodhibitiwa na wale wanaotumia lugha ya kifaransa.
Berliner Zeitung
Nalo gazeti la Berliner Zeitung wiki hii linatema sumu kwa viongozi kadhaa wa barani Afrika na watoto wao linasema kwamba watawala fulani wa Afrika wanajulikana duniani kwa tabia ya kutojali haki za binadamu, wanaiba mali za umma na wanang'ang'ania madaraka mpaka wanaanguka kwenye mimbari. Ni sawa kabisa kusema kwamba watawala hao ndio wanaosababisha bara la Afrika likwame lakini watoto wao wanavuka mipaka. Mfano ni Teodorin Obiang Mangae mtoto wa rais wa Guinea ya Ikweta Teodoro Obiang. Mtoto huyo anaouonyesha utajiri wake hadharani, miongoni mwa wanaserere wake wa kuchezea ni boti ya kifahari yenye thamani ya dola milioni 150 pamoja na msururu wa magari aina ya Limousine nyumba ya kifahari iliyopo mjini Paris yenye thamani ya Euro milioni mia moja.
Gazeti hilo la Berliner Zeitung pia linatufahamisha juu ya mwanamke tajiri kuliko wengine wote barani Afrika, Isabel dos Santos binti ya aliekuwa rais wa Angola Jose Eduardo Dos Santos aliyetawala Angola kwa muda wa miaka 38. Berliner Zeitung limeandika kuwa dada huyo Isabel dos Santos aliutumia utawala wa baba yake kujijengea utajiri wenye thamani ya dola bilioni 3.5 na yeye hivi sasa ni mkurugenzi mkuu wa kampuni ya mafuta ya Angola Sonangol.Isabel mwenye umri wa miaka 44 anashikilia kazi ya pili iliyo muhimu kabisa katika nchi hiyo ya pili kwa utajiri wa mafuta barani Afrika huku kaka yake Jose akiuongoza mfuko wa fedha wa serikali ya Angola (Fundo Soberano de Angola).
Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman