Afghanistan yazuia watu kutembea usiku
25 Julai 2021Mamlaka nchini Afghanistan zimetangaza kizuizi cha kutotembea nje nyakati za usiku katika majimbo 31 kati ya 34 nchini humo ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukabiliana na ongezeko la machafuko yaliyotokana na mashambulizi makubwa ya wanamgambo wa Taliban katika miezi ya hivi karibuni.
Taarifa hii ni kulingana na wizara ya mambo ya ndani nchini Afghanistan.
Kumeshuhudiwa ongezeko la uasi kutokana na mashambulizi ya wanamgambo wa Taliban ambao pia wamedhibiti mipaka muhimu, wilaya kadhaa na kuizingira baadhi ya miji mikuu ya majimbo tangu mapema mwezi Mei wakati muungano wa wanajeshi wa kigeni unaoongozwa na Marekani ulipoanza kuondoka nchini humo.
Taarifa ya wizara ya mambo ya ndani ya Afghanistan imesema "ili kukabiliana na machafuko na kuzuia vuguvugu la wanamgambo wa Taliban kumeanzishwa zuio la watu kutotembea nje kwenye majimbo 31 nchini humo," kasoro Kabul, Panjshir na Nangarhar.
Watu hawataruhusiwa kutembea kuanzia saa nne usiku hadi saa kumi za alfajiri kwa saa za nchini Afghanistan, amesema msemaji wa wizara hiyo ya mambo ya ndani Ahmad Zia Zia, kwenye taarifa ya sauti iliyosambazwa kwa waandishi wa habari.
Wakati wanajeshi hao wa kigeni wakiwa bado hawajamaliza kuondoka nchini humo, tayari wanamgambo wa Taliban wanadhibiti karibu nusu ya takriban wilaya 400 za Afghanistan.
Mashambulizi yaanza upya baada ya Idd al-Adha.
Mashambulizi yalitulia kwa muda wiki hii wakati Waislamu walipokuwa wakiadhimisha sikukuu ya Idd al-Adha, lakini yameanza tena, huku mamlaka zikidai kuwa zimefanikiwa kuwaua zaidi ya wanamgambo 260 wa Taliban katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita, kwenye baadhi ya majimbo.
Soma Zaidi: Mapambano na Taliban yashika kasi Afghanistan
Hata hivyo taarifa hizi hazijaweza kuthibitishwa.
Wakati mashambulizi yakiwa yameshika kasi katika wiki za karibuni, jeshi la Marekani lililazimika kufanya mashambulizi ya kutokea angani katika kile kilichoelezwa kama kulisaidia jeshi la Afghanistan kukabiliana na mashambulizi ya wanamgambo wa Taliban, hata katika wakati ambapo wanakaribia kukamilisha mchakato wa kuondoka nchini humo, msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani John Kirby alisema siku ya Alhamisi.
Wataalamu wanasema kukosekana kwa msaada wa mara kwa mara wa jeshi la Marekani kushambulia kutoka angani tangu mwezi Mei kumechangia kwa kiasi kikubwa kwa wanajeshi wa Afghanistan kupoteza majimbo mengi kwa Taliban.
Mashirika: AFPE