1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zuma katuvunja moyo - Upinzani Burundi

Hamida Issa26 Februari 2016

Upinzani nchini Burundi unamlaumu Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini ambaye, akiwa kiongozi wa ujumbe wa marais watano wa Afrika, ametaka suala la muhula wa tatu wa Rais Pierre Nkuruniziza madarakani lisijadiliwe.

https://p.dw.com/p/1I2ph
Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini anayeongoza ujumbe wa marais watano wa Afrika nchini Burundi akiwa na Rais Pierre Nkurunziza (kulia).
Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini anayeongoza ujumbe wa marais watano wa Afrika nchini Burundi akiwa na Rais Pierre Nkurunziza (kulia).Picha: Reuters/E. Ngendakumana

Mkutano kati ya marais hao na viongozi wa chama tawala na wa upinzani mjini Bujumbura hapo jioni ya jana (Februari 25) unaonekana kuwa ulimalizika pasi na makubaliano ya kimsingi. Tayari mmoja wa marais hao wa Afrika, Ali Bongo wa Gabon, ameshaondoka nchini Burundi.

Mkutano huo uliokusudia kuweka msukumo kwenye jitihada za kumaliza mzozo unaoikabili Burundi uliwajumuisha pia wajumbe wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na viongozi wa dini.

Licha ya kuwa upande wa chama tawala (CNDD-FDD) haukutowa taarifa yoyote juu ya matokeo ya mazungumzo yao, wafuasi wa vyama vya upinzani vinasema vimevunjwa moyo. Kiongozi wa chama cha UPRONA, ambacho hakikubaliani na serikali ya Rais Nkurunziza, anasema ujumbe wa marais hao watano wa Afrika haukufanya chochote cha maana.

"Tumevunjika moyo. Hakuna hatua yoyote iliyopigwa kuhusiana na nia ya Umoja wa Afrika ya kumaliza mgogoro unaoikabili nchi. Rais Zuma anasema swala la muhula wa tatu si la kujadiliwa kwani ni korti ya kikatiba iliruhusu muhula huo wa tatu, wakati sote tunaelewa ni katika mazingira gani korti ya kikatiba iliupitisha uamuzi huo," alisema mwanasiasa huyo, huku akiutuhumu ujumbe huo kwa kuja kumuunga mkono tu Rais Nkurunziza na muhula wake wa tatu.

Kwa upande wake, mkuu wa chama FRODEBU, Leonce Ngendakumana, ambaye pia anaongoza muungano wa vyama vya upinzani, anasema waliwataka marais hao wauone umuhimu wa mazungumzo yanayoshirikisha pande zote.

"Tunashuhudia silaha zilivyotapakaa nchini na pia uundwaji wa makundi ya kijeshi. Walituuliza endapo kuna njia nyingine ya kuimaliza hali hiyo, nasi tuliwahakikishia kuwa hakuna isipokuwa majadiliano. Kwa hiyo, lazima majadiliano yafanyika na hayo wanaotajwa kuwa waliendesha mapinduzi."

Nkurunziza hataki kuzungumza na 'magaidi'

Awali Rais Nkurunziza alishasema wazi kuwa hayuko tayari kuzungumza na wale aliowaita "magaidi" wanaouhujumu usalama wa Burundi, akimaanisha muungano wa wapinzani wake wanaoishi nje ya nchi hiyo na ambao wanatajwa kuhusika na jaribio la mapinduzi lililoshindwa mwezi Mei 2015.

Hata hivyo, kabla ya kuondoka mjini Bujumbura hivi leo, Rais Bongo wa Gabon alisema kuwa wameafikiana majadiliano yataendelea kufanyika na kuwashirikisha wote.

"Kilichoafikiwa baada ya kuzisikiliza pande zote ni kuwa lazima kuwepo na mazungumzo. Ni kupitia njia hiyo tu, ndipo utulivu unapoweza kurudi katika nchi hii", alisema Rais Bongo.

Mbali na Rais Bongo, ujumbe huo uliotumwa na Umoja wa Afrika na unaongozwa na Rais Zuma wa Afrika Kusini, unawajumuisha pia Waziri Mkuu wa Ethiopia, Haile Mariam Deseleyn, Rais Mohamed Ould Abdelaziz wa Mauritania na Macky Sall wa Senegal.

Kauli ya mwisho juu ya matokeo ya mazungumzo hayo inatarajiwa leo kutolewa leo na Rais Zuma, ambaye mchana huu anafanya mazungumzo na Rais Nkurunziza.

Mwandishi: Hamida Issa/DW Bujumbura
Mhariri: Mohammed Khelef