1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiUganda

Zoezi la sensa Uganda laanza na malalamiko ya wafanyakazi

Lubega Emmanuel10 Mei 2024

Zoezi la sensa ya watu ambalo hufanyika kila baada ya miaka kumi limeanza hii leo nchini Uganda chini ya kiwingu cha shutuma na lawama kutokana na kile kimetajwa kuwa matayarisho duni.

https://p.dw.com/p/4fhK1
Uganda Kampala | Umwelt | Kampf gegen Altkleider
Picha: Badru Katumba/AFP

Baadhi ya maafisa walioshiriki mafunzo ya  kuendesha zoezi la sensa Uganda ambalo limeanza Alhamisi usiku wanalalamika kuwa hawajapokea vitendea kazi ikiwemo kifaa cha kidijitali cha kurikodi taarifa kutoka kwa raia. Isitoshe hawana sare wala vitambulisho kuweza kukaribishwa majumbani mwa watu ambao wamesalia makwao wakisubiri kuhesabiwa.  Serikali ilitangaza Ijumaa kuwa siku ya mapumziko kwa ajili ya sensa.

Soma pia: Rais Museveni wa Uganda akutana na wafanyabiashara Kampala

Kile kinachoshangaza na kuleta kero ni kwamba shirika husika la takwimu hapa Uganda UBOS lilianza maandalizi ya zoezi hili miaka 9 iliyopita mara tu baada ya kukamilisha zoezi la awamu ya tano lililofanyika mwaka 2014. Ni kwa msingi huu ndipo hata wamiliki wa vyombo vya habari na utangazaji kupitia shirikisho la  NAB wamekataa kurusha matangazo ya bure ya kuhamasisha raia kushiriki zoezi hilo ikiwa hakuna bajeti ya kuwalipa. Waziri wa habari Chris Baryomunsi amewarai wamiliki vya vyombo vya habari wazingatie maslahi ya kitaifa kwa wakati huu kwa sababu zoezi hilo ni muhimu sana kwa kila mtu. Amesema. "mwito wangu ni kwamba kwa mujibu wa maslahi ya kitaifa pamoja na ushirikiano wa serikali wa kila mara vyombo vya habari rusheni ujumbe huo"

Rais wa Uganda Yoweri Museveni
Rais wa Uganda Yoweri Museveni Picha: Darko Vojinovic/AP Photo/picture alliance

Kulingana na shirika la takwimu la  UBOS, mkuu wa familia atatakiwa kuwa nyumbani wakati wa zoezi hilo likifanyika. Hii ni sababu anatarajiwa kujibu maswali kadha wa kadha kuanzia muundo wa familia yake yaani ana watoto na wake wangapi na kadhalika, Pia atatakiwa kuelezea kuhusu njia na hali zake za kimapato zinazomwezesha kukidhi mahitaji ya watu wanaomtegemea.

Lakini baadhi ya watu wanapinga maswali kama hayo wakielezea kuwa si vyema kwa serikali kutaka kujua kuhusu maisha binasfi ya mtu kwa kiwango hicho. Wanahofia kuwa taarifa hizo zaweza kutumia kuwaandama. Kwa sasa Uganda inakadiriwa kuwa na watu milioni 48 na wengi huishi vijijini. Matokeo ya sensa yatathibitisha idadi kamili ya watu.