Zoezi la kuhamisha raia Aleppo kuanza tena
16 Desemba 2016Taarifa za awali zilieleza kuwa zoezi hilo limesimamishwa baada ya wapiganaji wanaoiunga serikali kutaka majeruhi kuondolewa kutoka kwenye vijiji vinavyokaliwa na waislamu wa madhehebu ya Shia ambavyo vilizingirwa na wapiganaji wa makundi ya waasi.
Maafisa hao wanasema zoezi hilo halijakamilika, na bado kuna raia wengi ambao bado wamesalia Aleppo. Ikiwa ni siku ya pili ya kuwahamisha raia na wapiganaji kutoka Mashariki mwa mji wa Aleppo limesimamishwa wakati ambapo kumeibuka madai kutoka pande zinazokinzana. Urusi ilisema jeshi la Syria limeimarisha udhibiti wake kwenye maeneo yote ya Mashariki mwa Aleppo, ingawa majeshi hayo yameendeleza mashambulizi kwenye maeneo yaliyotengwa ambayo waasi wanaendelea kuyapigania.
Vyanzo vya habari kutoka upinzani vinawashutumu wapiganaji wa Kishia kwa kushambulia mabasi yaliyokuwa yakihamisha raia kutoka Aleppo na vizuizi ambavyo viliwekwa na kuyalazimu mabasi hayo kurejea Aleppo. Hatua hiyo ilisababisha waasi nao kuanzisha mashambulizi, amesema afisa mmoja wa waasi.
Afisa kutoka jeshi la Syria amesema, zoezi hilo la kuhamishwa raia lilisimamishwa kufuatia madai ya waasi waliotaka kuwarejesha watu waliowateka, lakini pia walitaka kuchukua silaha zilizokuwa zimefichwa kwenye mabegi, madai ambayo yamepingwa vikali na makundi ya waasi yenye makao yake mjini Aleppo.
Urusi na Uturuki kuanzisha mazungumzo mapya ya amani Syria.
Awali, Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema, yeye pamoja na mwenzake Rais wa Uturuki, Tayipp Erdogan wanashirikiana pamoja kuandaa mfululizo wa mazungumzo mapya ya amani ya Syria bila ya kuwahusisha Marekani na Umoja wa Mataifa. Putin ametoa kauli hiyo leo hii akiwa Japan, kwenye mkutano na waandishi wa habari.
Amesema hatua hiyo ni pekee kwa ajili ya Uturuki na Urusi na iwapo itafikiwa itakuwa ni sehemu ya makubaliano ya umoja wa Mataifa yanayoendelea mjini Geneva.
Hatua hiyo inayoelezwa kuwa haikutarajiwa inaonyesha kuongezeka kwa msukumo wa mashirikiano kati ya Urusi na Uturuki, baada ya kudorora kufuatia tuhuma za Uturuki kuitungua ndege ya Urusi mwaka jana, lakini pia ikionyesha nia ya Urusi ya kuongeza ushawishi wake kwenye eneo la Mashariki ya kati na kwingineko.
Huku hayo yakiendelea, chanzo cha habari kutoka upande wa waasi kimearifu kwamba kundi la Jabhat Fateh al-Sharm, ambalo awali lilitambulikana kama Nusra Front, wamekubali kuondolewa kwa majeruhi kutoka kwenye eneo lililozingirwa la vijiji vya madhehebu ya kishia vya Foua na Kefraya, vilivyoko jimbo la Idlib. Hatua hii ikiruhusu zoezi la kuwahamisha raia na wapiganaji kuendelea.
Wakati kundi hilo la mwisho la waasi likikubali kuondolewa kwa majeruhi, afisa mmoja wa Syria amesema zoezi hilo sasa litaanza mara moja. Awali waasi walisema wamekubaliana kuondolewa kwa majeruhi kutoka Foua na Kefraya kama sehemu ya makubaliano ya kuwahamisha wapiganaji na raia kutoka Mashariki mwa Aleppo.
Mwandishi: Lilian Mtono.
Mhariri: Grace Patricia Kabogo