1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zimbabwe: Mnangagwa atangaza baraza jipya la mawaziri

1 Desemba 2017

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa ametangaza baraza lake jipya la mawaziri. Maafisa wakuu wa jeshi na makada wa chama tawala cha ZANU PF ndio wamepewa nafasi katika baraza hilo lenye mawaziri 22.

https://p.dw.com/p/2oaJ0
Simbabwe Emmerson Mnangagwa in Harare, 2014
Picha: picture-alliance/AP Photo/T. Mukwazhi

Wakosoaji  nchini Zimbabwe wanasema fungate fupi baada ya harusi imemalizika na ukweli wa mambo sasa unadhihirika, kilichotarajiwa ni kwamba Rais Emmerson Mnangagwa angelichanganya baraza lake, lakini kuna ishara chache mno za mabadiliko. Akizungumza na waandishi habari muda mfupi kabla baraza jipya la mawaziri kutangazwa, kiongozi mkuu wa upinzani Morgan Tsvangirai alisema Mnangagwa alikuwa na nafasi ya kuonyesha kuwa yeye ni tofauti na Mugabe lakini hapakuwepo na majadiliano yoyote baina yao na uongozi huo mpya.

Ishara haba za mabadiliko

Tsvangirai anasema hakuna mabadiliko hadi sasa na jambo ambalo linatia wasiwasi ni jinsi rais mpya alivyoanza. Tsvangirai amesema kuna wasiwasi juu ya msingi anaojaribu kuuweka rais huyo mpya wa Zimbabwe katika kuyashughulikia mambo na kutoa mpango madhubuti wa kufufua uchumi.

Morgan Tsvangirai kiongozi mkuu wa upinzani wa Zimbabwe
Kiongozi mkuu wa upinzani wa Zimbabwe Morgan TsvangiraiPicha: Getty Images

Mnangagwa amemchagua meja jenerali Sibusiso Moyo, kamanda wa jeshi ambaye wiki mbili zilizopita alitangaza kwenye televisheni hatua ya wanajeshi ya kuingilia kati baada ya nchi hiyo kukabiliwa na mkwamo wa kisiasa hatua ambayo hatimaye wiki iliyopita ilisababisha kuufikisha mwisho utawala wa kiongozi maarufu wa zamani wa nchini Zimbabwe Robert Mugabe. Rais huyo mpya pia amempa nafasi ya uwaziri wa ardhi na kilimo jemadari Perrance Shiri aliyehudumu kwa muda mrefu kwenye kikosi cha jeshi la anga la Zimbabwe.

Chinamasa arejea katika wizara ya fedha

Kulingana na taarifa zilizotolewa rais Mnangagwa hata hivyo amewabakisha mawaziri wachache kutoka kwenye baraza la zamani la aliyekuwa rais wa nchi hiyo Robert Mugabe miongoni mwao ikiwa ni Patrick Chinamasa ambaye amerudishwa kuhudumu kama waziri wa fedha, wizara aliyokuwa anaishikilia kabla ya kuondolewa wakati Mugabe alipofanya mabadiliko katika baraza la mawaziri manamo mwezi Oktoba.

Meja jenerali Sibusiso Moyo wa jeshi la Zimbabwe
Meja jenerali Sibusiso MoyoPicha: Reuters/ZBC

Chris Mutsvangwa kiongozi wa mashujaa katika harakati za ukombozi wa Zimbabwe za mwaka 1980 na aliyeongoza katika juhudi za kumlazimisha Mugabe aachie madaraka ndiye waziri mpya wa habari. Hata hivyo rais Mnangagwa hakuwajumuisha wapinzani katika baraza hilo la Mawaziri.

Wakili mmoja ambaye pia ni mkosoaji Alex Magaisa aliweka kwenye mtandao wake wa Tweeter picha ya rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe na mkewe Grace wakiwa wanacheka pamoja na ujumbe wa maneno uliosema "pale walipoliona baraza la mawaziri”.

Biti: Kipindi cha fungate kimekwisha

Naye aliyekuwa zamani waziri wa fedha Tendai Biti ameandika ujumbe kwenye Tweeter uliosema kipindi cha fungate kimekwisha hata kabla hakijaanza na kumalizia kwa kusema "Ni aibu! Ni sawa na kupoteza nafasi adimu”.

Mnangagwa, mwenye umri wa miaka 75, aliapishwa Ijumaa iliyopita baada ya matukio makubwa katika nchi hiyoya kusini mwa Afrika pale jeshi lilipoidhibiti nchi ya Zimbabwe na kusema walitaka kuwakamata wahalifu katika serikali waliokuwa wanamzunguka Mugabe mwenye umri wa miaka 93.

Mwandishi: Zainab Aziz/ AFPE/p.dw.com/p/2oa5H

Mhariri: Grace Patricia Kabogo