1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zimbabwe: Mnangagwa asema ng'o haundi serikali ya umoja

5 Januari 2018

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa amemtembelea nyumbani kwake kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai ambaye anasumbuliwa na maradhi ya saratani lakini amesema hatua hiyo si ishara ya kuundwa kwa serikali ya umoja.

https://p.dw.com/p/2qPeM
Simbabwe Emmerson Mnangagwa Rede in Harare
Picha: Reuters/P. Bulawayo

Ziara ya rais Mnangagwa imefanyika wakati ambapo vyama vya kisiasa nchini Zimabwe vinajiandaa kuanza kampeni za uchaguzi hapo baadae katika mwaka huu. Kampeni hiyo ya uchaguzi nchini Zimbabwe itakuwa ni ya kwanza tangu kujiuzulu kutoka madarakani kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Robert Mugabe baada ya jeshi kutwaa udhibiti wa nchi hiyo.

Makamu wa rais wa Zimbabwe - Constantino Chiwenga
Makamu wa rais wa Zimbabwe Constatino ChiwengaPicha: picture alliance/AP/dpa/T. Mukwazhi

Katika ziara yake ya kumtembelea kiongozi wa upinzani rais Mnangagwa aliandamana na makamu wake Constantino Chiwenga, aliyekuwa zamani mkuu wa jeshi na ambaye aliongoza mapinduzi baridi ya mwezi Novemba mwaka jana.

Kuhusu hali ya kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai rais wa Zimbabwe amesema  anaendelea kupata ahueni na kwamba hivi karibuni atapelekwa nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kupata matibabu zaidi. Bwana Tvangirai aligundulika kuwa ana saratani ya utumbo mkubwa baada ya kufanyiwa uchunguzi miaka miwili iliyopita.

Naibu wa Tsvangirai katika chama cha upinzani cha Movement for democrati Change (MDC) Nelson Chamisa amesema rais Mnangagwa ametoa ishara inayotakikana katika masuala ya kisiasa ikiwa ni pamoja na siasa za amani na zile za kila mmoja kumjali mwenziwe.

Kiongozi wa upinzani wa Zimbabwe Morgan Tsvangirai
Kiongozi wa upinzani wa Zimbabwe Morgan TsvangiraiPicha: Getty Images

Tsvangirai aliwahi kuwa waziri mkuu katika serikali ya umoja nchini Zimbabwe kati ya mwaka 2009 na 2013 baada ya kumzidi kwa kura mtangulizi wa Mnangagwa, rais wa zamani Robert Mugabe katika duru ya kwanza ya uchaguzi uliofanyika mwaka 2008, lakini hakupata kura za kutosha ili kuzuia duru ya pili ya uchaguzi. Hata hivyo alisusia duru hiyo kwa madai kwamba wanajeshi walichochea vurugu dhidi ya wafuasi wake. Katika serikali ya umoja Tsvangirai alionekana kuwa ni waziri mkuu asiye na nguvu kutokana na ushawishi mkubwa aliokuwa nao rais Robert Mugabe

Muungano wa upinzani umemchagua kiongozi huyo Morgan Tsvangirai kama mgombea wake katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu wa 2018 ili kupambana na chama kinachotawala cha ZANU PF chini ya uongozi wa rais Emerson Mnangagwa.

Bila shaka uchaguzi wa mwaka huu utakuwa ni mtihani mkubwa kwa rais mpya wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa katika hatua ya kuhalalisha uongozi wake.

Mwandishi:Zainab Aziz/AFPE/APE/RTRE

Mhariri: Gakuba, Daniel