Zimbabwe kuidhinisha rasimu ya katiba
16 Machi 2013Chama kikuu cha upinzani nchini humo, ikiwa ni pamoja na chama tawala cha rais Mugabe cha ZANU-PF , vinaunga mkono rasimu hiyo ya katiba na kufanya wingi wa wastani unaohitajika kupitisha rasimu hiyo kwa kura ya "Ndio" kuwa na uhakika.
Shambulio dhidi ya wanaharakati na maafisa wa chama cha Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai katika mkesha wa kura hiyo ulichafua kile ambacho , kwa viwango vya Zimbabwe, ni kampeni ambayo haikuwa na umwagikaji wa damu.
Licha ya kuwa maafisa wameyalenga makundi yanayopendelea demokrasia katika wakati wa kuelekea upigaji kura leo Jumamosi(16.03.2013) na kuwakamata viongozi wao pamoja na vifaa, vifo vichache vimeripotiwa.
Wafuasi washambuliwa
Katika shambulio la siku ya Ijumaa, wafuasi wa chama cha Tsvangirai cha Movement for Democratic Change, MDC, walipigwa wakati wakiweka mabango wakiwahimiza wapiga kura kuidhinisha rasimu hiyo.
Chama cha MDC kimedokeza kuwa shambulio hilo limefanywa na waungaji mkono wa chama cha Rais Mugabe cha Zimbabwe African National Union- Patriotic Front.
Polisi walipuuzia tukio hilo kuwa limepangwa na kundi la wafanyakazi wa televisheni ya BBC, ambao pia wameshambuliwa, "kuionyesha Zimbabwe kuwa ni nchi ya ghasia".
Madaraka ya rais yatapungua
Katiba mpya itapunguza madaraka ya rais ambayo Rais Mugabe alikuwa nayo katika kipindi cha miaka 33 ya utawala wake na kuweka misingi ya uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika Julai mwaka huu, uchaguzi ambao utafikisha mwisho makubaliano ambayo mara nyingi yameingia katika matatizo ya kugawana madaraka kati ya Mugabe na Tsvangirai.
Licha ya kuwa mswada huo wa katiba unaungwa mkono na Mugabe mwenye umri wa miaka 89 na hasimu wake Morgan Tsvangirai mwenye umri wa miaka 61, hali ya wasi wasi kati ya waungaji mkono wa vyama hivyo viwili vikuu unatokota baada ya chaguzi kadha nchini humo zilizosababisha umwagikaji wa damu.
"Mashambulio hayo ni ushahidi wa wazi kuwa ZANU_PF inataka kufanya vitendo vya ghasia," amesema msemaji wa chama cha MDC Douglas Mwonzora.
Katika uchaguzi wa mwaka 2008 zaidi ya watu 180 waliuwawa na wengine 8,000 walijeruhiwa, kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International , na kuzusha hali ya kuporomoka kwa uchumi wa taifa hilo hali iliyomlazimisha Mugabe kukubali kugawana madaraka na Tsvangirai.
Wengi wanaiangalia hatua ya serikali ya kuwakera wanaharakati kabla ya kura hiyo ya maoni kuwa ni hatua ya mwanzo ya kuelekea katika ukandamizaji mkubwa wakati wa uchaguzi.
Wazimbabwe watakiwa kupiga kura kwa amani
Mkuu wa tume ya uchaguzi nchini Zimbabwe , ZEC, ambaye ameteuliwa hivi karibuni , Rita Makarau, jana Ijumaa aliwasihi wananchi kupiga kura kwa amani.
"Tafadhalini nendeni kupiga kura kwa amani , hii ni sheria yetu kuu," amesema Makarau.
Kiasi ya watu milioni sita wanatarajiwa kupiga kura leo katika vituo vya kupigia kura nchini humo.
Rasimu hiyo ya katiba ambayo ilitarajiwa kukamilika katika muda wa miezi 18 ilichukua miaka mitatu kukamilika.
Tvangirai , ambaye amekuwa akifanya mikutano karibu kila siku, amewataka viongozi wa kidini nchini humo kuomba dua kwa ajili ya nchi hiyo, ambayo ilikuwa moja kati ya nchi tajiri katika bara la Afrika lakini majaaliwa yake yameporomoka kwa sasa.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Grace Patricia Kabogo