Ziara ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa ujerumani Mashariki ya kati
24 Novemba 2009Mkutano wa kilele wa hali ya hewa mjini Copenhagen na ziara ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani,Guido Westerwelle nchini Israel ndizo mada zilizohanikiza magazetini hii leo.
Tuanze lakini na ziara ya waziri wa mambo ya nchi za nje Guido Westerwelle Mashariki ya kati na hasa nchini Israel.Gazeti la Mannheimer Morgen linaandika:
Westerwelle anatambua kishindo kinachomkabili waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani anapoitembelea Israel.Yadhihirika hata hivyo hali hiyo haimsumbuwi.Hata kabla ya kuanza ziara yake hiyo,Westerwelle aliwatonesha waisrael aliposema ujenzi wa makaazi ya wayahudi ndio kizingiti kikubwa katika utaratibu wa amani.Na ili kuondowa uwezekano wa kuzuka dhana ,waziri wa mambo ya nchi za nje amesisitiza jukumu la aina pekee la Ujerumani kwa Israel.Hata hivyo,si mageni kwa yeyote yule kwamba shirikisho la jamhuri ya Ujerumani,miaka 60 baada ya kuundwa Israel,halijitokezi kama wakili wa dola hilo la kiyahudi tuu,bali pia linatilia maanani masilahi ya wapalastina ,kwa namna ambayo msimamo wake unaweza kuaminika.Hiyo ndio njia pekee inayoifanya Ujerumani isifiwe na pande zote mbili kama mpatanishi wa kuaminika,kwa mfano katika majadiliano ya mpango wa kuachiwa huru wafungwa kati ya Israel na Palastina.
Gazeti la Rhein-Neckar-Zeitung la mjini Heidelberg linaandika:
La,ziara ya Guido Westerwelle mjini Jerusalem si ya kumezewa mate.Takriban kila anachokifanya,ataambiwa amefanya sivyo-machache tuu ndio anayoweza kuambiwa amefanya sawa.Machache hayo hayo ndiyo aliyofanikiwa kuyatekeleza mnamo siku ya kwanza ya ziara yake hapo jana.Waziri wa mambo ya nchi za nje ameandika ndani ya daftari la kumbukumbu za wahanga wa mauwaji ya halaiki ya Holocaust-Jad Vaschem,"jukumu letu liko pale pale na urafiki wetu unakua".Matamshi ya busara.Matamshi yanayoweza pia kutafsiriwa kama kuomba radhi kwa matamshi ya chuki dhidi ya wayahudi yaliyotolewa wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2002 na Jürgen Mölleman.
Mada yetu ya pili magazetini inahusu mkutano wa kilele wa hifadhi ya hali ya hewa mjini Copenhagen.Gazeti la Märkische Allgemeine la mjini Postdam linaandika:
Kwa kweli watu wasiuwekee matarajio makubwa mkutano wa kilele wa Copenhagen.Hali ya kumaizi na dhamiri njema ni nadra kupatikana au hakuna kabisa katika majukwaa ya kisiasa.Na bila ya shaka madai ya nchi za magharibi ni ya haki kwamba sehemu iliyosalia ya dunia nayo pia ikubali hesabu zao za kiuchumi zichunguzwe bila ya mapendeleo na pasiwepo yeyote atakaejaribu kutumia mbinu na hadaa kuficha viwango vya moshi unaotoka viwandani.Sote wa kutoka eneo tajiri la kaskazini ya dunia tutabidi kulipia mabilioni kwaajili ya kuhifadhi hali ya hewa na madhara yanayotokana na mabadiliko ya hali ya hewa.Ndio maana kuna umuhimu wa kuchunguza fedha hizo zinatumika ipasavyo ,kuweza kuleta tija inayotakikana na kwa hivyo kuepukana na balaa la fedha hizo kutumbukia mahala kusikojulikana.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir (Inlandspresse)
Mhariri:Abdul-Rahman