Ziara ya Hillary Clinton nchini Angola, anaelekea DRC.
10 Agosti 2009Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton anawasili mchana huu nchini jamhuri ya kidemokrasi ya Congo akitokea nchini Angola ambako ametoa mbinyo kwa serikali ya Angola jana , kuchukua hatua zaidi katika mapambano yake dhidi ya ufisadi wakati wa ziara ya siku mbili katika nchi hiyo inayotoa mafuta kwa wingi ziara iliyokuwa na lengo la kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.
Pamoja na kugusia masuala ya rushwa na ufisadi, Clinton amemtaka kiongozi wa muda mrefu wa Angola kufanya uchaguzi, na kukaa imara katika kuimarisha demokrasia katika taifa hilo la kusini mwa Afrika ambalo mafuta yake yanatakiwa na wengi.
Clinton amekuwa waziri wa mambo ya kigeni wa kwanza wa Marekani kukaa usiku mzima nchini Angola, nchi ambayo inashindana na Nigeria katika bara la Afrika katika sekta ya nishati lakini ni nchi ambayo theluthi mbili ya wakaazi wake wanaishi kwa kipato cha chini ya dola mbili kwa siku.
Alikutana na viongozi wa juu na maafisa wa ngazi ya juu katika sekta ya uzalishaji mafuta katika taifa hilo ambalo lilikuwa hasimu katika enzi za vita baridi, na ambayo inaipatia China mafuta mengi na kumekuwa na ongezeko la ushawishi wa China nchini humo.
Lakini wakati China inajizuwia kuzungumzia masuala ya haki za binadamu, Clinton ameyagusia katika mkutano na waandishi habari, akimtaka rais Jose Erduardo Dos Santos ambaye ameiongoza Angola tangu nchi hiyo kupata uhuru kutoka Ureno mwaka 1975 , kufanya uchaguzi wa rais.
Clinton amesema kuwa ametiwa moyo , kwamba Angola imefanya uchaguzi wa amani na wenye kuaminika wa bunge mwaka jana, ukiwa wa kwanza katika muda wa miaka 16.
Angola ambayo iko katika nafasi ya 158 katika orodha ya shirika la Transparency International kuhusiana na rushwa duniani kutoka mataifa 180, ina uhusiano mzuri na Marekani na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton amelizungumzia hilo.
Rushwa na ufisadi limekuwa suala muhimu katika ziara ya Clinton katika bara la Afrika, akisisitiza msimamo wa rais Barack Obama wakati alipotembelea nchini Ghana mwezi uliopita. Ameisifu Angola kwa kuchapisha mapato yake yatokanayo na mafuta katika mtandao na kufanyakazi pamoja na maafisa wa Marekani katika kuimarisha uwazi.
Clinton anawasili leo mjini Kinshasa , jamhuri ya kidemokrasi ya Congo ambako suala kuu litakuwa kuitaka nchi hiyo kuchukua hatua za kumaliza matumizi ya nguvu dhidi ya wanawake.
Clinton kesho atakwenda mjini Goma , mashariki ya Congo ambako kuna wakimbizi wengi kutokana na miaka 15 ya mapigano katika eneo hilo, na ataweza kuwafariji baadhi ya wanawake walioathirika na matumizi ya nguvu na kubakwa na kuitaka nchi hiyo kuchukua hatua kumaliza hali hiyo.
Mwandishi Sekione Kitojo/AFPE/RTRE.
Mhariri Mohammed Abdul-Rahman
►◄