Zelensky ziarani Slovakia kabla ya kuelekea Uturuki
7 Julai 2023Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine aliwasili katika mji mkuu wa Slovakia, Bratislava kabla ya kuelekea Uturuki ambako pia anatazamiwa kufanya mazungumzo na Rais Recep Tayyip Erdoga leo. Ziara yake Slovakia aliitangaza mwenyewe kupitia katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter.
Mada kuu kwenye mkutano wake alioufanya na rais Zuzana Caputova ni kutafuta kungwa mkono zaidi kijeshi na dhamira ya kujiunga na Umoja wa Ulaya pamoja na Jumuiya ya kujihami ya NATO. Rais Caputova ni kati ya viongozi wa Ulaya walio mstari wa mbele katika kuiunga mkono Ukraine.
Rais huyo ameshawahi kuitembelea Kyiv mara mbili tangu ilipoingia kwenye mzozo na Urusi na amewahi kuyatembelea maeneo ambayo yameathiriwa zaidi na mgogoro huo akiwa sambamba na Zelensky.
Katika ziara mkutano wao wa leo, Zelensky pia ameitolea wito jumuiya ya kujihami ya NATO ishughulikie masuala ya azma ya Sweden na Ukraine kujiunga na jumuiya hiyo na kuongeza kuwa, kutokuwa na uamuzi kuhusu suala hilo kunatishia uimara wa jumuiya hiyo na usalama wa dunia.
Wanachama wa NATO kuungana kuisaidia Ukraine kujiunga na jumuiya hiyo
Katika hatua nyingine, katibu mkuu huyo wa jumuiya ya kujihami ya NATO Jens Stoltenberg amesema kuwa mkutano wa wiki ijayo wa jumuiya hiyo utatafuta njia ya kuisaidia Ukraine kuwa mwanachama.
Stoltenberg amezungumzia pia suala la kupeleka silaha tata, zinazopingwa na makundi ya haki za binadamu za mabomu ya mtawanyiko. Amesema, ni juu ya washirika binafsi kuamua ni aina gani ya wanapaswa kupeleka Ukraine.
Wakati huo huo, vyombo vya habari vya Urusi vimeripoti kwamba, serikali ya nchi hiyo inafikiria kufanyika kwa mkutano kati ya rais Vladimir Putin na mwenzake wa Urusi, Recep Tayyip Erdogan, ingawa bado tarehe maalumu kwa ajili ya tukio hilo haijapangwa.