Zelensky: Urusi itashindwa kama Manazi wa Ujerumani
8 Mei 2023Christoph Heubner, Naibu kiongozi wa Kamati ya Auschwitz, amesema leo kuwa watu wengi walionusurika kutokana na ukatili wa viongozi wa kinazi wa Ujerumani walichukulia kitendo cha kuangamizwa kambi za mateso na kukombolewa kama ushindi mkubwa na walitumaini kwa dhati kwamba Ulaya ingeliachana kabisa na vita na ingepata fundisho juu ya vitendo vya ukatili, mateso na uhalifu.
Ama kuhusu uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, Heubner amesema, wahanga hao ambao kwa sasa ni vikongwe, wanaishi kwa hofu kubwa kutokana na vita vinavyoendelea barani Ulaya na ambavyo bila shaka vinawakwaza na kuzusha kumbukumbu mbaya.
Wakati wa kumbukumbu ya miaka 78 ya kujisalimisha kwa Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema Urusi itashindwa kama walivyoshindwa manazi wa Ujerumani.
"Kwa kupinga maadili yetu, adui huyu ambaye ni Urusi kwa mara nyingine tena ameweka msisitizo kwenye uchokozi na uvamizi, mauaji ya watu wengi na mateso. Kushambulia miji na vijiji kwa mabomu. Bado hatujajua tarehe ya ushindi wetu, lakini tunajua hii itakuwa sherehe kwa Ukraine, kwa Ulaya yote, na kwa ulimwengu wote ulio huru."
Mnamo Mei 8, mwaka 1945, mataifa washirika walikubali hatua ya Ujerumani kujisalimisha bila masharti baada ya kushindwa vita. Siku hiyo, inayojulikana kama Siku ya Ushindi barani Ulaya, husherehekewa kwa gwaride na sherehe zingine. Nchini Urusi na katika nchi nyingine zilizokuwa zamani za Muungano wa Kisovieti, siku hiyo huadhimishwa Mei 9. Kamati ya Auschwitz ilianzishwa na wahanga wa kambi ya mateso na maangamizi dhidi ya Wayahudi ya Auschwitz-Birkenau, nchini Poland.
Ulaya kuyawekea vikwazo makampuni ya China
Hayo yanajiri wakati ambapo Umoja wa Ulaya umependekeza vikwazo kwa makampuni ya China yanayotuhumiwa kuuza vifaa vinavyoweza kutumiwa katika uundwaji wa silaha na hivyo kuisaidia Urusi katika vita vyake nchini Ukraine. Hayo yameripotiwa jana na Jarida la the Financial Times.
Ripoti hiyo imebaini ikinukuu nakala ya jarida hilo kuwa makampuni saba ya China yameorodheshwa katika kifurushi kipya cha vikwazo ambavyo vitajadiliwa na nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya mapema wiki hii.
Hii leo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China Wang Wenbin amesema Beijing inatoa wito kwa Umoja wa Ulaya kuepuka kuchukua "muelekeo usiofaa", vinginevyo China itachukua hatua madhubuti kulinda haki na maslahi yake.