Zelensky: ajali ya ndege inayodaiwa kumuua Prigozhin
24 Agosti 2023Shirika la habari la Ukraine, Interfax limemnukuu leo Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akisema kuwa nchi yake haihusiki kwa vyovyote vile na ajali hiyo inayodaiwa kusababisha kifo cha Prigozhin. ''Kwanza kabisa hatuhusiki, huo ndiyo ukweli. Nadhani kila mtu anatambua aliye nyuma ya ajali hiyo,'' alisisitiza Zelensky
Kifo cha Prigozhin ni manufaa kwa Kiev
Zelensky amewaambia waandishi habari kuwa kifo cha Prigozhin ni manufaa kwa Kiev, kwa namna fulani. Inaaminika kuwa kiongozi huyo wa Wagner na kamanda wa ngazi ya juu wa kundi hilo, Dmitri Utkin walikuwa ndani ya ndege binafsi ya kampuni ya Prigozhin, ambaye aliongoza uasi dhidi ya jeshi la Urusi miezi miwili iliyopita.
Hata hivyo, hadi sasa Ikulu ya Urusi, Kremlin na wizara ya ulinzi ya Urusi, hazijazungumzia tukio hilo, wala kuthibitisha kuhusu kifo chake. Mshauri wa Rais Zelensky, Mykhailo Podolyak ameliambia gazeti la Ujerumani la Bild kuwa kifo cha Prigozhin, aliyekuwa na umri wa miaka 62 kilikuwa kinatabirika. Kulingana na Podolyak, kiongozi huyo wa Wagner alisaini hati yake ya kifo, mara tu alipofanya uasi.
Hayo yanajiri wakati ambapo uchunguzi wa ajali hiyo unaendelea. Wachunguzi wa ajali ya ndege leo wamechukua mabaki ya ndege hiyo na wameanzisha uchunguzi wa jinai, lakini hakuna taarifa rasmi ambayo inaeleza kile kilichosababisha ndege hiyo kuanguka.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Poland, Mateusz Morawiecki amesema kundi la Wagner litazidi kuwa hatari, kwa sababu litakuwa chini ya uongozi wa Rais wa Urusi, Vladimir Putin. Matamshi hayo ameyatoa leo wakati akizungumza na waandishi habari mjini Warsaw.
Wagner ilichangia Urusi kushinda baadhi ya maeneo ya Ukraine
Kundi la mamluki la Wagner lilichangia kwa kiasi kikubwa Urusi kupata ushindi katika baadhi ya maeneo Ukraine. Hata hivyo, lilipata hasara kubwa mashariki mwa Ukraine, wakati walipochukua maeneo ya Popasna, Soledar na Bakhmut, na hivyo kuiharibu miji hiyo katika mapambano yao.
Abbas Gallyamov, aliyekuwa mwandishi wa hotuba za Rais Putin, ambaye kwa sasa amegeuka na kuwa mkosoaji wake mkubwa amesema bila kutoa ushahidi, kuwa kiongozi huyo wa Urusi anahusika na ajali hiyo ya ndege. Gallyamov ameandika katika mtandao wa kijamii wa Telegram kwamba sasa ni wazi mtu hawezi kumpinga Putin, kwani ana nguvu za kutosha na anaweza kulipiza kisasi.
(AFP, DPA, Reuters)