Zelensky awasilisha ''mpango wa ushindi'' kwa washirika
10 Oktoba 2024Mazungumzo hayo ya pande tatu yaliyofanyika Alhamisi kwenye ofisi za waziri mkuu wa Uingereza ya Downing Street, kujadiliana kuhusu hali ya vita Ukraine, yamehudhuriwa kwa pamoja na Starmer, Zelensky na Katibu Mkuu wa Jumuia ya Kujihami ya NATO, Mark Rutte.
Msaada zaidi wahitajika
Zelensky anatafuta kuongeza msaada wa kijeshi na kifedha katika ziara yake barani Ulaya. Rais huyo wa Ukraine amesema mpango huo una lengo la kuanzisha mazingira sahihi ya kukomesha vita kwa kuzingatia haki. Amesema wamekubaliana kulifanyia kazi kwa pamoja na washirika wao.
Zelensky ameshikilia msimamo wake kwamba Ukraine bado inahitaji sana msaada zaidi ili kupambana na Urusi ambayo imeiteka miji kadhaa midogo na vijiji katika eneo la mashariki linalozozaniwa.
Katika mkutano huo, Zelensky aligusia ajenda ya Ukraine kuruhusiwa kutumia makombora ya masafa marefu iliyopewa na washirika wake, ikiwemo makombora ya Uingereza chapa Storm Shadow, ili kuyashambulia maeneo ya kijeshi ya Urusi. Marekani na Uingereza zimejizuia kutoa idhini ya kutumika silaha hizo, kwa hofu kwamba inaweza kuwaingiza washirika wa NATO kwenye mzozo wa moja kwa moja na Urusi.
Kwa upande wake Rutte amesema hawalizungumzii suala hilo kwa sababu ya ukweli kwamba wanataka kuiunga mkono Ukraine, lakini pia kwa sababu ya kuiunga mkono Ukraine katika vita vyake dhidi ya Urusi, ni muhimu kwa usalama wa Ulaya, Canada, Marekani na kwenye nchi zote wanachama wa NATO.
Putin kuingia Ukraine ni hatari kwa NATO
''Kwa sababu, ikiwa Putin atafanikiwa kuingia Ukraine, hilo lingemaanisha athari kubwa ya usalama. Litakuwa na athari kubwa ya usalama kwa sisi sote katika NATO,'' alifafanua Rutte.
Baada ya kumaliza ziara yake Uingereza, Zelensky amewasili Paris, Ufaransa, kama sehemu ya ziara yake hiyo ya Ulaya kutafuta uungwaji mkono zaidi wa mataifa ya Magharibi, ambayo itampeleka hadi Roma, Italia na Berlin, Ujerumani. Akiwa mjini Paris, Zelensky amekutana na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron.
Wakati huo huo, Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine Oleksiy Kuleba amesema Urusi iliishambulia miundombinu ya bandari ya Ukraine kwa karibu mara 60 katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita. Kuleba amesema Urusi pia inazidisha mashambulizi kama hayo, ambayo madhumuni yake ni kupunguza uwezo wa mauzo ya nje ya Ukraine.
Soma zaidi: Mapigano zaidi yaripotiwa mashariki mwa Ukraine
Amesema wanazungumzia kuhusu kuchochea kwa makusudi mzozo wa chakula katika sehemu hizo za ulimwengu ambazo zinategemea moja kwa moja usambazaji wa nafaka za Ukraine. Kulingana na Kuleba, mashambulizi hayo yameharibu takribani miundombinu 300 ya bandari na meli 22 za kiraia.
Ama kwa upande mwingine, maafisa kwenye jimbo la Odessa wamesema Alhamisi kuwa idadi ya watu waliouawa katika shambulizi ya Urusi imefikia watu wanane.
(AFP, AP, DPA, Reuters)