Zelensky ataka NATO kujadili ulinzi wa anga wa Ukraine
17 Aprili 2024Akilinganisha hali ya Ukraine na ile ya Israel, baada ya shambulizi kubwa la Iran la makombora na droni kuzuiwa mwishoni mwa wiki, Zelensky amesema Ukraine itaomba kupewa mifumo ya ulinzi wa mashambulizi ya angani na makombora. Amesema Waukraine wana haki ya kulindwa dhidi ya ugaidi.
Rais huyo wa Ukraine alimpongeza Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz kwa kutafuta suluhisho la mzozo huo. Akizungumza na Rais wa China Xi Jinping mjini Beijing jana, Scholz alisisitiza umuhimu wa China kwenye jukwaa la kimataifa. Kama mshirika muhimu wa Urusi, Xi anaonekana kuwa na ushawishi kwa Rais wa Urusi Vladmir Putin.
Zelensky amesema China inaweza kusaidia kurejesha amani nchini Ukraine na utulivu katika uhusiano wa kimataifa. Uswisi itakuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele wa amani katikati ya mwezi Juni, ambao China imealikwa na wala sio Urusi.