Zelensky ataka majadiliano ya Ukraine kujiunga na EU yaanze
5 Novemba 2023Kufuatia ziara ya rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen mjini Kiev, rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky anatarajia majadiliano ya Umoja wa Ulaya ya kujiunga kwa taifa hilo katika Umoja huo kuanza mwaka huu.
Haya yanajiri baada ya Von der Leyen awali kukiri mafanikio ya Ukraine, ambayo imekuwa ikijilinda kufuatia uvamizi wa jirani yake Urusi kwa zaidi ya miezi 20.
Urusla amesema Ukraine imepata mafanikio makubwa katika lengo lake la kujiunga na Umoja wa Ulaya, akitaja mageuzi ya mfumo wa mahakama, kuzuwia ushawishi wa matajiri wa Urusi na vita dhidi ya utakatishaji fedha.
Zelensky alisema kwamba amesikia majibu na ishara nzuri kuhusu mchakato wa kuanza kwa majadiliano ya Ukraine kujiunga na Umoja huo.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kuamua kuhusu kuanza kwa mchakato huo katika mkutano wao wa Desemba.