Zelensky ahudhuria mkutano wa kuijenga upya Ukraine
11 Juni 2024Kiasi viongpozi, wanasiasa na maafisa 2,000 wa mashirika ya kimataifa wanahudhuria mkutano wa mjini Berlin unaowaleta pamoja watu kutoka maeneo mbalimbali ya ulimengu wanaojishughulisha na juhudi za maendeleoa na kuyejenga upya maeneo yaliyohabiriwa na vita nchini Ukraine. Mkutano huo hautarajiwi kuwa wa wafadhili unaonuia kuchangisha fedha.
Akizungumza kwenye mkutano huo, kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amewatolea wito washirika watoe msaada zaidi wa kijeshi kuisaidia Ukraine kuimarisha mfumo wake wa ulinzi wa anga dhidi ya mashambulizi ya Urusi. Scholz ameapa kwamba Urusi katu haitashinda vita vyake nchini Ukraine, akisema hakutakuwa na ushindi wowote wa kijeshi kwa rais wa Urusi Vladimir Putin wala amani ya kulazimishwa.
"Nguvu, uthabiti wa kanuni. Haya ni masharti kwa Putin kutambua kwamba hakutakuwa na ushindi wa kijeshi na hakuna amani iliyoamriwa. Ni lazima Putin afikishe mwisho kampeni yake ya kikatili na kuwaondoa wanajeshi wake," alisema Scholz.
Zelensky asema mfumo wa ulinzi wa anga ni jawabu la vita Ukraine
Kwa upande wake rais Zelensky amewahimiza washirika watoe mifumo zaidi ya ulinzi wa anga, akisema ndilo jawabu la kukomesha mafanikio ya uvamizi wa Urusi na kupata amani ya kudumu.
Zelensky aidha amesema uwezo mkubwa wa kimkakati iliyonayo Urusi kuipiku Ukraine ni ubora na nguvu zake katika anga. Zelensky amedokeza kuwa ni ugaidi wa makombora na mabomu ndio unaowasaidia wanajeshi wa Urusi kusonga mbele ardhini.
Rais huyo ameongeza kusema mashambulizi makombora na droni ya Urusi dhidi ya vituo vya nishati ya Ukraine yameharibu nusu ya uwezo wake wa kuzalisha umeme tangu majira ya baridi kali.
Soma pia: Ukraine yasema imeshambulia mifumo ya ulinzi wa anga ya Crimea
Ujerumani inaongoza juhudi za kuchukua hatua ya haraka kuimarisha ulinzi wa anga wa Ukraine na imeshatoa mifumo mitatu aina ya Patriot kwa serikali ya mjini Kyiv.
Mapema asubuhi Zelensky alikaribishwa mjini Berlin na rais wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier kabla kuanza kwa mkutano huo w akimataifa. Steinmeier alimpokea Zelensky katika makazi yake rais katika kasri la Bellevue na baadaye kuandamana naye kwenye mkutano. Baadaye mchana Steinmeier atahudhuria kikao cha bunge la Ujerumani ambako Zelensky atatoa hotuba.
(dpa, afp)