1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelenskiy ataka Urusi itimuliwe FAO

9 Juni 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy ametaka Urusi iwekewe vikwazo vya muda mrefu kwa kuchochea mzozo wa chakula duniani kwa kuzuwia usafirishaji wa nafaka kutoka bandari za Ukraine.

https://p.dw.com/p/4CUJd
75th Cannes Film Festival - Volodymyr Zelenskiy
Picha: Serge Arnal/Starface/IMAGO

Akiuhutubia kwa njia ya vidio mkutano wa kila mwaka wa shirika la ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo, OECD, Rais Zelenskiy amehimiza pia vikwazo vikali dhidi ya taifa hilo kwa kuzuwia bandari na kwa kuchochewa wimbi jipya la uhamiaji dhidi ya Ulaya.

Soma pia: Merkel atetea urathi wake wa Urusi, asema hataomba radhi

Pia ametoa wito wa kuondolewa kwa Urusi kutoka kwenye shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO, na kusema madhara ya vita vinavyoendelea dhidi ya nchi yake yanakwenda mbali ya Ulaya Mashariki kwa sababu shehena za nafaka kutoka Ukraine zimekwama nchini humo, na hivyo kupelekea kupanda kwa bei za chakula.

Ukraine | Weizenfeld in der Luhansk Region
Shamba na ngano lililopo karibu na kijiji cha Yubileiny, kilomita 2.5 magharibi mwa Lugansk, wilaya ya Lutuginsky.Picha: Alexander Reka/TASS/dpa/picture alliance

"Hatuwezi kuzungumzia kuendelea kwa uanachama wa Urusi katika FAO, shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa. Urusi inafanya nini ndani ya FAO ikiwa Urusi hiyo hiyo inasababisha njaa kwa watu wasiopungua milioni 400 na pia kwa zaidi ya watu bilioni 1?"

Soma pia: Zaidi ya raia elfu kumi wazuiliwa kuondoka Sievierodonetsk

Ukraine ni moja ya wasafirishaji wakubwa zaidi duniani wa ngano, mahindi na mafuta ya kupikia, lakini usafirishaji wa bidhaa hizo umesitishwa kwa sehemu kubwa na vita, na mzingiro wa Urusi wa pwani ya Ukraine ya bahari nyeusi. Takribani tani milioni 22 za nafaka zinaelezwa kusalia nchini Ukraine.

Mapambano makali yaendelea kuwani mji wa Sievierodonetsk

Hayo yanajiri wakati mapigano makali yakiendelea katika mji wa mashariki wa Sievierodonetsk kati ya vikosi vya serikali ya Ukraine na majeshi ya Urusi.

Ukraine-Krieg | Zerstörung in Bachmut
Mwanajeshi wa Ukraine akipita karibu na kiwanda cha gypsum kilichoharibiwa na mashambulizi ya Urusi mjini Bakhmut, mashariki mwa Ukraine.Picha: Francisco Seco/AP Photo/picture alliance

Vikosi vya Ukraine vimedai kusonga mbele katika mapigano ya mtaa kwa mtaa, lakini vinasema tumaini lao kubwa la kupata mafanikio ni kupitia kupatiwa mizinga na makombora yenye uwezo zaidi ili kukabiliana na nguvu kubwa ya jeshi la Urusi.

Soma pia: Ukraine yaendelea kushikilia 'maeneo' ya Sievierodonetsk

Katika upande wa kusini, wizara ya ulinzi ya Ukraine imesema imeteka maeneo mapya kufuatia mashambulizi ya kujibu mkoani Kherson, ikilenga eneo kubwa zaidi ambalo Urusi imeliteka tangu uvamizi wake mnamo mwezi Februari.

Mapigano katikati mwa magofu ya Sievierodonetsk, ambao ni mji mdogo wa kiviwanda, yamekuwa mmoja ya makali zaidi katika vita hiyo, huku Urusi ikielekeza uvamizi wake mjini humo. Pande zote zinasema zimetiana hasara kubwa.

Soma pia: Majeshi ya Urusi yaishambulia vikali miji ya mashariki mwa Ukraine

Huko mjini Brussels kwenye makao makuu ya Umoja wa Ulaya, wabunge wa bunge la umoja huo wamewatolea mwito viongozi wakuu wa mataifa wanachama wa kanda hiyo kuzifanya Ukraine na nchi jirani ya Moldova kuwa wagombea rasmi wa kujiunga na jumuiya hiyo.

Viongozi wa makundi ya kisiasa ndani ya bunge la Ulaya wamesema Umoja wa Ulaya unapaswa kuwa mshirika anaeaminika na kutimiza kanuni zake kwa kuonyesha mshikamano kwa wale wanaosimamia maadili sawa.

Chanzo: Mashirika