1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Zelenskiy aishukuru Poland kwa ushirikiano

6 Aprili 2023

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema Poland itasaidia kuunda muungano wa Magharibi wa kuipatia nchi yake ndege za kivita.

https://p.dw.com/p/4PmGK
Polen, Warschau | Staatsbesuch von Wolodymyr Selenskyj
Picha: Wojtek Radwanski/AFP/Getty Images

Haya yanajiri huku wanajeshi wake wanaendelea kutetea ngome yake ya mashariki Bakhmut inayokabiliwa na mashambulizi makali kutoka Urusi.

SOMA PIA: Zelensky awasili Poland kwa ziara ya nadra nje ya Ukraine

Rais Zelenskiy ametowa kauli hiyo wakati akiwa ziarani nchini Poland alikokwenda kuishukuru nchi hiyo kwa kusimama na Ukraine tangu kuanza kwa vita hivyo.

Zelenskiy amesema bado nchi yake ndiyo inayoudhibiti mji wa Bakhmut ambao Kiev inasema wanajeshi wake wamepambana na mashambulizi ya Urusi katika eneo la viwanda la mji huo.

Naibu wake wa ulinzi, Hanna Malyar, amesema kwamba hali katika mstari wa mbele wa mapambano imedhibitiwa licha ya majaribio ya mara kwa mara ya Urusi kujaribu kuutwaa mji wa Bakhmut na miji mingine mashariki mwa Ukraine.

Usambazaji wa silaha

Ukraine, Woltschansk | Eindrücke aus der Region Charkiw
Picha: Hanna Sokolova/DW

Lakini kuhusiana na upatiwaji wa ndege za kivita, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg, amesema utumaji wa aina yoyote ya misaada hatari kwa Urusi katika vita yake na Ukraine itakuwa kile alichokitaja kama "kosa kubwa la kihistoria lenye athari kubwa."

Kwa upande mwengine, Rais wa Ufaransa Emannuel Macron aliye ziarani sasa mjini Beijing, amesema kwamba China haina maslahi yoyote katika kutuma silaha nchini Urusi. Huku China yenyewe ikisema kwamba haina mipango hiyo na inaalaani utumaji wa silaha kutoka nchi za Magharibi kwa Ukraine.

Hayo yanakuja wakati Rais wa Urusi Vladimir Putin akiwaambia mabalozi wapya wa Marekani na Umoja wa Ulaya wanaoziwakilisha nchi zao mjini Moscow kwamba nchi zao zimehusika katika kuzorota kwa kasi kwa mahusiano tangu Urusi ilipotuma vikosi vyake nchini Ukraine mwaka jana. Putin aliyasema haya baada ya kuwakaribisha mabalozi hao nchini humo.

SOMA PIA: Makamu Kansela wa Ujerumani Robert Habeck afanya ziara ya ghafla nchini Ukraine

Aidha Putin alisema kuna sababu ya kuamini kwamba mashirika ya kijasusi ya nchi za Magharibi yalihusika katika kile alichokitaja kama hujuma na vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na Ukraine.

Kauli hizi zimejiri akizungumza katika mkutano wa baraza la usalama la Kremlin lililo na jukumu la kuhakikisha utulivu katika maeneo manne ya Ukraine ambayo Putin anadai kuyazingira mwaka jana.

Wakati huo huo Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi imelalamika kwamba nchi za Magharibi hazikuwa zimeonyesha wasiwasi wake juu ya mauaji ya mwanablogu wa kijeshi huko St Petersburg siku ya Jumapili, hatua ambayo Urusi imeiita kitendo cha kigaidi.

 

 

//Reuters, AFP