Zanzibar yawa mwanachama kamili wa CAF
16 Machi 2017Aidha, shirikisho la mpira wa miguu la Zanzibar litapiga kura katika masuala ya soka la bara hilo. Zanzibar ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini ina serikali yake, imepewa idhini hiyo leo kwa kauli moja katika mkutano mkuu wa mwaka wa CAF unaofanyika Addis Ababa, Ethiopia.
Rais wa Shirikisho la Kabumbu nchini Tanzania, Jamal Malinzi, alitoa wito kwa Zanzibar ikubaliwe kuingizwa katika shirikisho la CAF.
Zanzibar sasa itakuwa mwanachama kamili wa CAF, ambayo ina nchi wanachama 55, sawa na wanachama wa Shirikisho la Soka barani Ulaya, UEFA kama shirikisho kubwa katika mashirikisho sita ya soka ya Shirikisho la Kabumbu Duniani, FIFA.
Wakati huo huo, Ahmad Ahmad kiongozi wa shirikisho la soka nchini Madagascar amechaguliwa kuwa rais wa CAF. Ahmad amemshinda Issa Hayatou kwa kura 34 dhidi ya 20. Hayatou kutoka Cameroon ameiongoza CAF kwa zaidi ya miaka 29.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, AP
Mhariri: Saumu Yusuf