Kisiwa cha utalii kiangamizwacho na madawa ya kulevya
17 Februari 2017Hakim alikuwa akimtazama mwenzake aliyekuwa amelala chini akikumbukia jinsi gani na yeye siku yake ya mwanzo ilivyokuwa, alipoanza kuachana na madawa ya kulevya ya heroin.
"Ilikuwa inauma sana, mwili ulikuwa na maumivu makali. Siku ya mwanzo nilikuwa kama huyu kijana aliyelala pale."
Hakim ana umri wa miaka 51, amedhoofika mpaka nguo zake zinaonekana kuwa ni kubwa sana kwake, miguu yake imejaa makovu na sasa yupo katika matibabu.
Kila mmoja kati ya wagonjwa 20 waliopo katika nyumba ya matibabu ya utumiaji wa madawa ya Spartan amepitia adhabu hiyo kali ya maumivu katika mikakati ya kuuchana na madawa ya kulevya ya heroin.
Ndani ya nyumba hiyo kuna bango lililochujuuka linaloamrisha watumiaji madawa wafuate hatua 12 za kuachana na madawa ya kulevya.
Bango jengine pia linasema "Siku baada ya siku" na "pole pole ndio mwendo."
Sehemu hii ambayo sio mbali na mji mkongwe za Unguja iliyomo ndani ya kuta kubwa, na iliyozungukwa na mageti ya nyumba za tabaka la kati, hapo ndipo wale wazanzibari waliokata tamaa wanapokuja kutafuta msaada.
Utumiaji wa madawa Zanzibar ni ugonjwa ulioenea. Tokea miaka ya 1980, kisiwa hiki kimekuwa ndio sehemu kubwa ya upitishaji wa madawa ya heroin kuto Afghanistan kuingilia Afrika kupitia Bahari ya Hindi.
Lakini tokea 2010, kumekuwa na mikakati ya kupambana na uingizaji wa madawa hayo.
"Takwimu zinaonesha kuwa kuanzia kilo 200 mpaka 400 zilikamatwa ndani ya kipindi cha miaka michache", anasema David Dadge, msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Madawa ya Kulevya.
Kwa vile fukwe za Zanzibar huwa zimejitenga, kisiwa hiki hutumiwa sana katika upitishaji wa madawa ya kulevya. Ingawa madawa hayo mengi husafirishwa kuelekea njia za kusini kama inavyoitwa, ikimaanisha Afrika ya Kusini na ya kati, madawa hayo pia humalizikia katika soko la Zanzibar .
Jumah Abdul Zidikheiry, afisa wa ngazi ya juu anayeongoza uchunguzi na vita vya kukabiliana na madawa ya kulevya,
anasema kukabiliana na madawa ya kulevya sio rahisi. "Sio kama kukabiliana na malaria. Malaria utatafuta chandurua, au utapiga dawa na tatizo limekwisha. Utumiaji wa madawa unaathiri nchi, unaathiri kila kitu."
"Zanzibar inahitaji msaada kutoka nje kukabiliana na tatizo hili, labda kutoka Ulaya au Marekani. Kwa sababu swali hili la madawa linaathiri uchumi wa visiwa hikv na kuvunja jamii," anasema Zidikheiry.
Mwandishi: Najma Said/DW English
Mhariri: Daniel Gakuba