1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamilioni wamewachwa na ulemavu tangu kuanza kwa vita hivyo

Faiz Musa 15 Machi 2019

Zaidi ya watu laki tatu na elfu sabini wamefariki huku mamilioni wakiwachwa na ulemavu miaka minane sasa tangu kuanza kwa vita katika taifa la Syria mwaka 2011.

https://p.dw.com/p/3F98F
Syrien Zerstörung
Picha: picture alliance/AP Photo/K.Al-Issa

Ripoti ya shirika linalochunguza masuala ya haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake mjini London, Uingereza, lilisema limenakili kiasi cha raia laki moja na elfu kumi na mbili waliuliwa huku elfu ishirini na moja wakiwa ni watoto na elfu kumi na tatu wanawake.

Ripoti hiyo ilieleza kwamba kiasi cha watu 60,000 wameuwawa kutokana na mateso au mazingira magumu ndani ya magereza ambapo kiasi cha watu nusu milioni wako magerezani tangu kuanza kwa vita hivyo.

Kitengo cha masuala ya kibinadamu katika Umoja wa Mataifa kilieleza kwamba kiasi cha watu milioni 2 na laki 9 wanaishi na ulemavu mbalimbali kutokana na vita hivyo.

Libanon Flüchtlinge aus Syrien
Wakimbizi wakiwa katika kambi ya Arsal iliyoko LebanonPicha: picture-alliance/AP Photo/H. Malla

Vile vile utafiti uliofanywa mwaka 2017 hadi 2018 na kundi la kimataifa la Ufaransa linalojihusisha na ulemavu unaonyesha kwamba zaidi ya theluthi ya familia za Syria kila mmoja ina mtu aliyepata ulemavu kutokana na vita hivyo.

Nayo ripoti ya shirika lisilokuwa la kiserikali kutoka Marekani la CARE inaeleza kwamba vita hivyo vimesababisha kiasi cha watu milioni 13 kuyahama makaazi yao na wengine kuwa wakimbizi katika mataifa jirani. Kiasi ambacho ni zaidi ya ilivyokuwa katika Vita vya Pili vya Dunia.

Watoto milioni moja wamezaliwa tangu kuanza vita hiyo

Mwenyekiti wa shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi UNHCR alisema wengi wa wakimbizi wa Syria wanaopata hifadhi nchini Lebanon hawana usalama na wanategemea misaada kutoka mashirika ya kimataifa.

Serikali ya rais wa Syria Bashar Al-Assad inadaiwa kukiuka haki za binadamu kwa kuwatesa watu, kuwabaka na hata kuuwaua.

Bildergalerie syrische Flüchtlinge Wintereinbruch Januar 2015
Mkimbizi na mwanawe katika kambi ya Al-Karameh mpakani mwa Syria na UturukiPicha: Reuters/K. Ashawi

Ripoti ya shirika la umoja wa mataifa linalowahudumia watoto inaonyesha kwamba kiasi cha watoto milioni 5 wamezaliwa tangu vita hivyo kuanza 2011 na milioni moja kati yao wamezaliwa ndani ya kambi za wakimbizi katika mataifa ya nje.

Ripoti hiyo inaonyesha kwamba kiasi cha watoto milioni mbili na laki moja hawaendi shule na kati ya shule tatu moja imeharibiwa ama kubomolewa kabisa.

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la uratibu wa misaada ya kiutu, OCHA linaeleza kwamba kiasi cha watu milioni 13 wanahitaji misaada ya kiutu.

Lakini serikali ya Syria imeyaita wanafiki mataifa yaliyoweka ahadi ya kutoa dola bilioni saba kusaidia raia wa Syria ikisema mataifa hayo yanaendelea kuiwekea vikwazo serikali yake kwa hivyo ahadi za mataifa na mashirika hayo ya kimataifa yanayoongozwa na Umoja wa Ulaya ni kichekesho na pia inakasirisha.

(AFPE)