Zaidi ya watu 30 wauawa katika mashambulizi ya Sudan
13 Januari 2024Kundi la mawakili wa Sudan wanaounga mkono demokrasia limesema kuwa mapigano baina ya makamanda wawili hasimu nchini humo yamewaua zaidi ya raia 30, ikiwemo mashambulizi ya anga katika mji mkuu wa Khartoum.
Awali kundi hilo la mawakili wa dharura, lilisema katika taarifa yake kwamba watu 23 waliuawa siku moja kabla, na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mashambulizi ya angani kwenye wilaya Soba mjini Khartoum. Baadae waliongeza idadi ya watu 10 waliokufa katika mashambulizi mengine ya anga ikiwa ni pamoja na mjini Khartoum.
Bofya hapa: Jenerali wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan asema hakutakuwa na suluhu na wauaji wa watu wa Sudan
Kundi jingine la kamati ya upinzani limeripoti idadi kama hiyo likisema raia 10 waliuawa na mizinga katika maeneo ya makaazi na soko.
Mwakilishi wa shirika la kuwahudumia watoto UNICEF nchini Sudan Mandeep O'Brien amesema kwamba vita hivyo vinaweza kusababisha janga kubwa kwa watoto milioni 24 wa nchi hiyo.