Zaidi ya watu 13 wauwawa Iraq
31 Desemba 2013Kambi hiyo ambayo imekua mwiba kwa serikali ya Waislamu wa madhehebu ya Shia inayoongozwa na Waziri Mkuu Nuri al-Maliki tangu kuanza kwake mwaka mmoja uliopita kutokana na kile wanachokiona kwamba wanatengwa kwa tofauti ya kimemadhehebu.
Maliki ambaye yupo katika mpango wa kuwania awamu ya tatu katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Aprili, amesikika mara kadhaa akionesha nia ya wazi ya kuwasambaratisha waandamanaji hao, kwa kuwatuhumu kuchochea vurugu na kuwaficha wanamgambo wa mtando wa kigaidi wa al-Qaeda.
Polisi imesema vurugu zilianza pale ambapo mtu mwenye silaha alipokifyatulia risasi kikosi maalumu cha polisi kilichokuwa kikijaribu kuingia katika mji wa Ramadi, eneo la magharibi ambalo kambi hiyo ipo. Chanzo kimoja kilisema milio ya risasi na miripuko ilisikika katika baadhi ya maeneo ya mji huo. Watu wenye silaha waliharibu kabisa magari matatu ya polisi na kuwauwa polisi watatu huko upande wa kaskazini wa mji huo wa Ramadi.
Miili ya watu 10 waliouwawa ilikwenda kuhifdahiwa katika chumba cha maiti cha hospitali ya Ramadi. Katika eneo lingine la Falluja, watu wenye silaha walishambulia kikosi cha jeshi kilichokuwa katika doria, kwenye eneo la barabara kubwa ilikuwa ikielekea Ramadi.
Kauli ya serikali kuhusu operesheni hiyo
Msemaji wa wizara ya ulinzi, Luten Jenerali Mohammed al-Askari aliiambia televisheni ya taifa hilo kwamba uamuzi wa kusambarataisha kambi hiyo umetokana na makubaliano yaliyofikiwa na viongozi wa kikabila,viongozi wa serikali katika maeneo hayo na wizara ya ulinzi.
Baadhi ya polisi wengine wanasema mahema bado yapo katika eneo hilo pamoja na polisi na jeshi kuzingira eneo hilo. Umoja wa mataifa umetoa wito pande zote nchini Iraq kujizuia na kuendelea na machafuko. Katika taarifa yake mjumbe wa Umoja huo kwa Iraq Nickolay Mladenov ameonesha wasiwasi wake juu ya hali inayoendelea sasa katika eneo la Anbar na kutoa wito wa wote kuwa watulivu na kuzingatia mkataba wa maelewano ulifikiwa katika kipindi cha siku mbili zilizopita.
Hali imekuwa tete katika eneo la Anbar kwa siku kadhaa sasa. Jummosi iliyopita polisi walimtia mbaroni mbunge maarufu kutoka madhehebu ya Sunni, Ahmed al-Alwani katika eneo ambalo kulitokea mapigano ambayo pia yasibababisha kifo cha kaka yake. Hapo jana wabunge 44 walitangaza kujiuzulu na kushikilia pia kuachiwa huru kwa mbunge huyo.
Idadi kubwa ya Waislamu wa madhehebu ya Sunni wamekuwa wakilalamika kwamba Washia wanatawala kimabavu tangu kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo Saddam Hussein mwaka 2003. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa zaidi ya watu elfu nane wameuwawa mwaka huu pekee kutokana na machafuko nchini Iraq.
Mwandishi: Sudi MnetteRTR/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman