1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya visa 18,700 vya mpox vyagunduliwa barani Afrika

17 Agosti 2024

Takriban visa 18,737 vya maambukizi ya virusi vya homa ya nyani vimeripotiwa barani Afrika tangu mwanzoni mwa mwaka huu. Haya ni kulingana na Kituo cha kudhibiti na kuzuia magonjwa barani Afrika, (CDC).

https://p.dw.com/p/4jZwd
Dalili za maambukizi ya homa ya nyani kwenye mkono wa mgonjwa anayeendelea kupata matibabu ya ugonjwa huo katika picha iliyotolewa na CDC mnamo mwaka 1997
Dalili za maambukizi ya homa ya nyaniPicha: AP/picture alliance

Katika taarifa, kituo hicho cha Africa CDC,  kimesema kufikia sasa, visa 3,101 vya maambukizi yaliyothibitishwa na visa 15,636 vinavyoshukiwa vimeripotiwa katika nchi 12 wanachama wa Umoja wa Afrika, na kusababisha vifo 541 hii ikiwa asilimia 2.89 ya kiwango cha vifo.

Visa zaidi vya mpox vyaripotiwa mwaka 2024

Kulingana na Africa CDC , visa zaidi vya maambukizi vimeripotiwa tangu mwanzo wa mwaka huu kuliko mwaka wote wa 2023, ulioshuhudia jumla ya visa 14,383.

Soma pia:WHO yasema ni muhimu kujiandaa kudhibiti kusambaa kwa mpox

Idadi hiyo ya maambukizi inajumuisha aina tatu ya virusi vya homa ya nyani, ambapo moja kati ya hizo ni kirusi kipya na hatari zaidi cha Clade 1b kinachoweza kuambukiza zaidi na kilichopelekea Shirika la Afya Duniani(WHO) kutangaza siku ya Jumatano dharura ya afya ya kimataifa, ikiwa ni tahadhari ya juu zaidi ya shirika hilo.