Yemen Kusini yachafuka baada ya jaribio la uhuru
5 Mei 2020Hatua ya karibuni ya vuguvugu la wanaotaka kujitenga kutangaza utawala wao katika mji muhimu wa bandari wa Aden na majimbo mengine ya kusini inazidi kuziweka Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu kwenye pande kinzani katika mgogoro, ambao hivi sasa uko katika mwaka wake wa sita.
Kiongozi wa wanaotaka kujitenga, Aydarous al-Zubaidi, alitoa tangazo hilo akiwa Abu Dhabi, makao makuu ya utwala Umoja wa Falme za Kiarabu, katika ishara ya wazi kwamba taifa hilo linaunga mkono hatua hiyo.
Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarbu zimekuwa washirika katika muungano unaoendesha vita dhidi ya waasi wenye mafungamano na Iran wa kabila la Houthi, walioteka sehemu ya kaskazini ya Yemen mnamo mwaka 2014.
Lakini washirika hao wawili wana maslahi yanayokinzana kusini mwa Yemen, na wanaegemea pande hasimu.
Umoja wa Falme za Kiarabu unaunga mkono vuguvugu la wanaotaka kujitenga, huku Saudi Arabia ikiunga mkono serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa, ikiongozwa na rais aliyeko uhamishoni Abed Raboo Mansour Hadi.
Vita dhidi ya Wahouthi kuwa vigumu zaidi
Mpasuko unaozidi kusini mwa Yemen unaweza kuzuwia zaidi juhudi za Saudi Arabia kutafuta njia ya kutoka kwenye vita ghali na vinavyoonekana kuwa vigumu kuvishinda dhidi ya Wahouthi.
Saudi Arabia imeimarisha mkakati wake wa kujitoa katika miezi ya karibuni, ikiwemo kufanya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na waasi.
Mwezi uliopita, taifa hilo lilitangaza usitishaji mapigano wa upande mmoja, lakini mpango huo ulipuuzwa na Wahouthi wakiutaja kama njama, na mapigano yanaendelea.
Umoja wa Falme za Kiarabu wakati huo huo, unataka kuhakikisha usalama wa njia za meli kwenye ukanda wa bahari ya Shamu pamoja na eneo muhimu la Bab el-Mandeb nje ya pwani ya Yemen.
Umoja wa Falme za Kiarabu ni msafirishaji mkubwa wa mafuta na ndiyo makao makuu ya DP World, shirika kubwa duniani la meli na usafirishaji.
Kwa kuunga mkono vuguvugu la wanaotaka kujitenga, Umoja wa Falme za Kiarabu unahakikisha pia kuwa chama kinachoungwa mkono na Saudi Arabia cha Islah, ambacho ni tawi la Udugu wa Kiislamu nchini Yemen, hakitazidi kuwa na nguvu kubwa.
Umoja wa Falme za Kiarabu unapinga matawi ya udugu wa Kiislamu kote katika kanda ya Mashariki ya Kati.
Mmzozo wageuka kuwa wa uwakala
Fernando Carvajal, mwanachama wa zamani wa kamati ya wataalamu ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, alisema huu unageuka kuwa mzozo wa kiuwakala kati ya Umoja wa Falme za Kiarabu na Wasaudi.
Jaribio la kujitawala linakuja wakati ambapo nchi hiyo imo katika hatari ya mripuko mbaya wa virusi vya corona.
Yemen imethibitisha visa 21 tu vya virusi hivyo, ikiwemo vifo vitatu, na vingi vimeripotiwa katika mji wa Aden, kwa mujibu wa wizara ya afya ya serikali inayotambuliwa kimataifa.
Wakaazi wa Aden wamedai hospitali zilifunga milango baada ya wafanyakazi wa afya kuhofia kuambukizwa virusi huku wakiwa hawana vifaa vya kujikinga.
Shirika la afya duniani WHO, lilionya siku ya Jumamosi kwamba virusi vinaenea nchini Yemen na kwamba linajiandaa na uwezekano wa nusu ya wakaazi wa taifa hilo kuambukizwa.
Al-Zubaidi anaongoza Baraza la Mpito la Kusini, ambalo ni ushirika wa makundi yenye silaha nzito na yanayofadhiliwa pakubwa na Umoja wa Falme za Kiarabu tangu 2015.
Baraza hilo linataka kurejesha taifa huru la Yemen Kusini, lililokuwepo kuanzia 1967-1990. Mapigano ya Kusini yanaiacha serikali ya Hadi ikiwa katika nafasi dhaifu zaidi wakati ikipambana kumaliza mzozo wa Wahouthi.
Chanzo: AP