Xi Jinping: Mradi wa BRI uko katika mwelekeo sahihi
18 Oktoba 2023Kulingana na rais Xi Jinping, mataifa yanayoendelea yanatakiwa pia kunufaika na mradi huo wa miundombinu ya barabara na reli ulioanzishwa miaka 10 iliyopita, akisema mabadiliko ya kihistoria sasa yanaonekana kote ulimwenguni. Miongioni mwa wawakilishi kutoka mataifa zaidi ya 140 alikuwa rais Vladimir Putin wa Urusi.
Soma zaidi: Putin akutana na mwenyeji wake Xi Jinping katika mkutano wa mradi wa BRI mjini Beijing
Kwenye hotuba yake hii leo, Xi aliikosoa Marekani na mataifa ya Umoja wa Ulaya kama Ujerumani ambayo si wanachama wa mradi huo, lakini yameliwekea vikwazo taifa hilo ama kuzichunguza bidhaa zake na kuongeza kuwa vikwazo hivyo vya upande mmoja, vinazuwia ukuaji wa kiuchumi na kuvuruga mifumo ya ugavi.
Putin aliyezungumza baada ya Xi alianza kwa kuisifu BRI akisema mradi huo na ushiriki wa Urusi vimesaidia kupata suluhu ya pamoja katika masuala mbalimbali ya kikanda. Uwepo wa Putin kwenye mkutano huo ni ishara ya wazi kwamba Urusi itasalia kuwa mshirika wa karibu sana wa Beijing.
Baadhi ya washiriki wamtenga Putin
Hata hivyo baadhi ya wawakilishi wa mataifa ya magharibi walitoka wakati Putin alipokuwa akihutubia. Hii ni baada ya mataifa mengi kumtenga kufuatia uvamizi wake nchini Ukraine. Lakini pamoja na hayo, Xi amemuhakikishia ushirikiano zaidi Putin, walipokutana katika mkutano baina yao.
Katika hatua nyingine, Rais wa Sri Lanka Ranil Wickremesinghe amesema unafuu wa madeni katika nchi za kipato cha chini unapaswa kuwa sehemu ya mabadiliko kuelekea uchumi wa kijani. Amesema kuwa kutokuchukua hatua katika suala la madeni kunaweza kuwa kitisho kikubwa kwa mradi wa miundombinu ya barabara na reli.
Rais huyo wa Sri Lanka amesema mpango wa ustawi wa hali ya hewa wa nchi yake unahitaji uwekezaji wa dola za Kimarekani bilioni 26.5 hadi kufikia mwaka 2042 na mkakati wa kutekeleza sera ya kuondoa hewa ya ukaa utapaswa kutumia dola bilioni 100 kufikia mwaka 2050.