1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Xi: China na Marekani zapaswa kuwa washirika, sio washindani

26 Aprili 2024

Rais wa China Xi Jinping amemuambia Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Antony Blinken, kwamba pande hizo mbili zinapaswa kuwa washirika kwenye masuala mbalimbali ya kikanda na kilimwengu na sio kuwa washindani.

https://p.dw.com/p/4fEeD
China | Antony Blinken akutana na Xi Jinping
Rais Xi Jinping wa China (kulia) akimkaribisha Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Antony Blinken, mjini Beijing.Picha: Mark Schiefelbein/REUTERS

Siku ya Ijumaa (Aprili 26), Rais Xi alifanya mazungumzo na mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Marekani, ambaye aliwasili mjini Beijing kukutana na viongozi wa China kujadiliana masuala kadhaa baina yao, ya kikanda na ya kilimwengu.

Kwenye mazungumzo yao, Rais Xi alisisitiza kwamba China na Marekani lazima zijihusishe zaidi na kusaka muafaka kuliko kuingia kwenye ushindani usiokwisha.

"China inafurahia kuiona Marekani yenye kujiamini, iliyo wazi, yenye maendeleo na inayosonga mbele. Tunatazamia na Marekani nayo inaweza kuyaangalia maendeleo ya China kwa mtazamo chanya. Hili ndilo jambo la msingi ambalo lazima lizungumzwe vyema." Alisema rais huyo wa China.

Soma zaidi: Blinken akutana na rais wa China Xi Jinping mjini Beijing

Blinken aliwaambia waandishi wa habari baada ya mazungumzo yake na Rais Xi kwamba, miongoni mwa mengine, alikuwa amekwenda Beijing kuwasilisha wasiwasi wa Marekani juu ya uungaji wa China kwa Urusi, ambayo uvamizi wake dhidi ya Ukraine umedumu kwa zaidi ya miaka miwili sasa.

Vile vile, waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani alisema kuwa yeye na rais huyo wa China walijadili masuala ya Taiwan, mzozo wa Bahari ya China Kusini, haki za binaadamu na utengezaji na usafirishaji wa vifaa vya teknolojia ya mawasiliano.

Matumaini ya kuimarika uhusiano

Baada ya mkutano wake wa leo, Blinken alionesha matumaini kwamba kumekuwapo na maendeleo kwenye uhusiano wa China Marekani, akitaja maeneo ya mawasiliano ya kijeshi, vita dhidi ya madawa ya kulevya, na pia ushirikiano kwenye teknolojia ya akili ya kubuni, ambapo alisema walikubaliana kuanzisha mdahalo juu ya kudhibiti hasara ya teknolojia hiyo inayokuwa kwa kasi.

China, Beijing | Mkutano wa Wang Yi na Antony Blinken
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa China, Wang Yi (kulia), akimkaribisha mwenzake wa Marekani, Antony Blinken, mjini Beijing.Picha: Mark Schiefelbein/POOL/AFP/Getty Images

"Tumekubaliana kudumisha na kuimarisha mawasiliano yetu ili kuendeleza mbele ajenda hii, na kisha kushughulikia tafauti zetu kwa umakini huku tukiepuka suintafahamu, dhana potofu, wala mahisabu yoyote mabaya." Alisema Blinken.

Soma zaidi: Blinken aanza ziara yake China

Hata hivyo, Blinken alisisitiza kuwa daima Marekani ingeliyalinda yale aliyoyaita "maslahi na maadili" yake, akielezea wasiwasi wake juu ya China kuipatia Urusi vifaa na mashine, ambavyo anaamini vimemsaidia Rais Vladimir Putin kwenye vita vyake dhidi ya Ukraine.

Awali, Blinken alifanya mazungumzo ya muda mrefu na mwenzake wa China, Wang Yi, na Waziri wa Usalama, Wang Xiaohong, ambapo wote walisisitiza umuhimu wa kufungua milango yao kwa ajili ya mawasiliano ya mara kwa mara na huku wakielezea masikitiko yao kwa kuendelea kwa tafauti zao, ambazo walisema zinatishia usalama wa dunia.

Tafauti hizo ziliibuka tena mapema wiki hii, baada ya Rais Joe Biden wa Marekani kusaiini muswaada wa sheria kuhusu msaada kwa mataifa ya kigeni, ambao China inauchukulia kuwa na matatizo, hasa kwa kuihusisha kwake Taiwan.

Lakini, licha ya tafauti kubwa baina ya Washington na Beijing, pande hizo mbili zimekuwa zikifanya mikutano ya ngazi za juu ya mara kwa mara katika siku za hivi karibuni. 

Vyanzo: AFP, AP